DAR ES SALAAM: WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamewafuata wapinzani wao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Gaborone United huku wakisema wanajivunia ubora wa kikosi chao cha msimu huu.
Kupitia taarifa ya klabu hiyo leo, Simba itapitia Afrika Kusini kuelekea Botswana ikisema iko imara, kiwango kilichooneshwa na wachezaji katika mchezo wa ngao ya jamii kinaridhisha na kinawapa nafasi ya kwenda kufanya vizuri kimataifa.
Msemaji wa Simba Ahmed Ally baada ya mechi dhidi ya Yanga waliyopoteza bao 1-0 alisema licha ya timu hiyo kupoteza mchezo wake, wanajivunia kiwango bora cha wachezaji wao na kwamba matokeo hayalingani na ubora waliouonesha uwanjani.
Alisema Simba ilitawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi, lakini changamoto ilikuwa ukosefu wa umakini katika kuzitumia hivyo, anaamini benchi la ufundi litafanyia kazi mapungufu madogo yaliyoonekana ili kuwa imara zaidi.
“Nikiri kuwa katika mechi zote tulizopoteza kwa mtani, hatujawahi kuwa na kiwango bora kama sasa. Hii imeonesha wazi timu iko imara na haina presha,” alisisitiza.
Ahmed pia aliwapa pole mashabiki wa Simba akiwataka wasikate tamaa kwa kupoteza mara kwa mara, akibainisha kuwa nguvu na malengo yao kwa sasa yameelekezwa kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
“Niwape pole mashabiki wetu, wasijisikie wanyonge. Hii ni mara ya sita kupoteza lakini hakuna sababu ya kuhesabu tumefungwa mara ngapi. Kiwango kiko juu na timu iko imara,” alisema.
Alisema safari bado ni ndefu kwenye mashindano ya ndani, akisisitiza kwamba wana imani kubwa ya kufanya vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba inatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone Septemba 20, mwaka huu, ambapo wamedhamiria kupata matokeo chanya ili kufanikisha safari ya kuingia hatua ya makundi.
The post Simba yajivunia ubora, yawafuata Gaborone first appeared on SpotiLEO.