DAR ES SALAAM: MAKAMU wa Rais wa Yanga SC, Arafat Haji, amesema siri ya mafanikio ya klabu hiyo kuanza vizuri msimu mpya inatokana na nidhamu, utulivu na kuheshimu dhamana waliyokabidhiwa na Watanzania.
Kauli hiyo inakuja baada ya Yanga kushinda bao 1-0 dhidi ya watani zao Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Haji alisema Yanga inaliona jukumu ililopewa na mashabiki wake kama deni kubwa linalopaswa kulipwa kwa matokeo chanya na kuwapa furaha.
“Nidhamu, utulivu na kuheshimu dhamana tuliyopewa na Watanzania wengi sana ndiyo msingi wetu. Ni lazima tuhakikishe Watanzania hao ambao wametuamini wanazidi kupata furaha na amani,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa kila msimu klabu hiyo imekuwa ikifanya makubwa na msimu huu umeshaanza vizuri, hivyo matarajio ni kuendelea kuandika historia kubwa zaidi.
Hata hivyo, baada ya mchezo huo Yanga ilianza safari za kwenda Angola kuifuata Wiliete kwa ajili ya mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Ijumaa ya wiki hii.
The post Yanga yataja siri ya mafanikio yao first appeared on SpotiLEO.