NEWCASTLE: MENEJA wa Barcelona Hansi Flick anategemea mshambuliaji wake Marcus Rashford ataongeza kasi wakati Wakatalunya hao watakapoanza kampeni ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Newcastle leo, wakati ambao kikosi hicho kinamkosa kinda Lamine Yamal kutokana na jeraha.
Rashford, ambaye alitoa ’assist’ wakati Barcelona ilipoichakaza Valencia mabao 6-0 Jumapili iliyopita, amevutia macho ya kocha huyo Mjerumani tangu awasili kwa mkopo kutoka Manchester United.
“Ninamfuatilia sana Marcus (Rashford) tangu aanze kuitumikia United. Na kila mara nilisema, ‘Wow!’ Ni bonge la mchezaji. Ana kasi, lakini pia akili yake kwenye ‘one against one’ ni kubwa mno, ni ya ajabu sana. Anavyomalizia mipira eneo la hatari ni ajabu sana.
“Nilichoona kwake katika wiki zake za kwanza hapa, ni kizuri sana. Nadhani bado ana uwezo mkubwa zaidi wa kutuonesha.” – Flick alisema katika mkutano na waandishi wa Habari.
Yamal, ambaye alianza msimu kwa kasi akiwa na mabao mawili na asisti mbili kwenye LaLiga, atakosa pambano hilo la usiku wa leo kutokana na jeraha la nyonga akiwa na timu ya taifa ya Hispania. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 pia anaweza kukosekana kwenye mechi ya Jumapili dhidi ya Getafe.
Barcelona watamkosa pia Alejandro Balde, Gavi, pamoja na Marc-Andre ter Stegen ambaye hayupo kwa muda mrefu, ingawa Frenkie de Jong anaweza kuwa fiti kuwatumikia mabingwa hao wa LaLiga.
The post Flick ampa Rashford viatu vya Yamal first appeared on SpotiLEO.