DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Karate Tanzania (TSKF) limeandaa semina ya kimataifa ya siku mbili kwa wachezaji na waamuzi wa mchezo huo nchini, ikiongozwa na bingwa wa zamani wa Ulaya, Shihan Tarabeih, ambaye ni mwalimu wa kiwango cha juu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika Karate.
Semina hiyo inatarajiwa kufanyika Septemba 19 na 20 mwaka huu katika ukumbi wa Upanga Club jijini Dar es Salaam, karibu na ubalozi wa Indonesia na Japani.
Akizungumzia mafunzo hayo leo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Karate Tanzania, Jerome Mhagama, alisema inalenga kuongeza ujuzi kwa timu ya taifa, walimu wa klabu mbalimbali na majaji wa mchezo huo nchini.
“Tumebeba gharama zote kama shirikisho ili kuhakikisha wadau wote wa Karate nchini wanapata nafasi ya kushiriki. Tutakuwa na mafunzo ya wachezaji, walimu na pia semina maalumu kwa majaji na waamuzi,” alisema Mhagama.
Kwa mujibu wa ratiba, semina hiyo itahusisha vipengele vya Kihon (mbinu za msingi), Kata (maumbo ya mapambano), Kumite (mapigano ya vitendo) pamoja na kliniki ya waamuzi ya kuimarisha maamuzi ya michezo.
Mhagama aliongeza kuwa ujio wa Shihan Tarabeih, utakuwa chachu ya maendeleo ya Karate nchini na kuongeza morali kwa wachezaji wanaoandaliwa kushiriki mashindano ya kimataifa.
“Tunawakaribisha wadau wote wa Karate, hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kujifunza moja kwa moja kutoka kwa gwiji wa dunia,” alisisitiza Mhagama.
The post Gwiji wa Karate Ulaya kuinoa Tanzania first appeared on SpotiLEO.