BERLIN: MSHAMBULIAJI wa Byaern Munich Harry Kane amesema Ligi ya Mabingwa ulaya (UCL) inatoa nafasi nyingi za kufunga kuliko Bundesliga baada ya mpachika mabao huyo wa England kupachika mabao mawili katika ushindi wa 3-1 wa Bayern Munich dhidi ya Chelsea jana Jumatano.
Nyota huyo raia wa England alifunga mkwaju wa penalti dakika ya 27 baada ya kuangushwa na kiungo wa Chelsea Moises Caicedo, kisha akatumia shinikizo la wachezaji wenzake kwa beki Malo Gusto kufunga bao la pili kwenye ‘far post’ dakika ya 63.
“Siku zote nahisi kama kwenye Champions League kuna wepesi wa kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga mabao kuliko Bundesliga, michezo iko wazi zaidi. Natumai naweza kupata zaidi ya mabao 11 msimu huu” – Kane alikiambia kituo cha utangazaji cha DAZN.
Kane mwenye umri wa miaka 32 tayari amefunga mabao tisa katika michezo mitano kwenye michuano yote msimu huu akiwa na Bayern mabao 10 katika michezo sita ikiwemo German Supercup.
Bayern walipata bao la kwanza dakika ya 20 ya mchezo huo, bao la kujifunga kutoka kwa Trevoh Chalobah na huenda wangefunga zaidi dhidi ya timu ya Chelsea ambayo ilionekana kukosa nguvu kadiri mchezo ulivyokuwa ukiendelea.
The post UCL nyepesi kwa Harry Kane first appeared on SpotiLEO.