CAPE TOWN: TIMU ya taifa ya Afrika Kusini itachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kukatwa pointi kwa kumchezesha mchezaji aliyefungiwa kwenye mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia mwezi Machi mwaka huu na kuweka matumaini yao ya kufuzu fainali hizo za mwaka ujao hatarini.
Shirikisho la soka Duniani FIFA wiki hii lililiarifu Shirikisho la Soka la Afrika Kusini kwamba linafungua jalada la uchunguzi kutokana na kumchezesha kiungo Teboho Mokoena katika mechi ya ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Lesotho.
Mokoena hakupaswa kucheza kwa sababu tayari alikuwa na kadi mbili za njano katika mechi hizo za kufuzu na alilazimika kukosa mechi hiyo kama tararibu za kinidhamu za FIFA zinavyoeleza.
Afrika Kusini ilikiri kufanya makosa hayo, lakini kuchelewa kwa FIFA kufungua jalada la uchunguzi kulisababisha miezi kadhaa ya uvumi kuwa huenda suala hilo limefunikwa Pia kulikuwa na ukosoaji wa chinichini kwa FIFA katika kutatua suala hilo kutoka nchi zingine zinazopigania nafasi ya juu katika kundi la Afrika Kusini.
Kanuni za nidhamu za FIFA zinasema: “Iwapo timu itamchezesha mchezaji ambaye hastahili kucheza (kutokana na kusimamishwa/kadi za njano, nyekundu), masuala ya usajili, uraia, n.k.), mechi itakuwa si halali. Matokeo ya msingi ni kupoteza mchezo kwa mabao 3-0, isipokuwa kama matokeo ya mchezo husika yatakuwa mabaya kwa timu yenye kosa (kama ilifungwa).”
Kupunguzwa pointi tatu kutaiacha Afrika Kusini sawa na Benin yenye pointi 14 kileleni mwa Kundi C zikiwa zimesalia mechi mbili za kufuzu kwa kila moja, huku Nigeria na Rwanda zikiwa nyuma kwa pointi tatu.
Ni washindi wa kundi pekee wanaofuzu moja kwa moja kwa fainali hizo za Amerika Kaskazini Juni ijayo. Raundi mbili za mwisho za mechi hizo zitachezwa mwezi ujao ambapo Afrika Kusini itakuwa ugenini dhidi ya Zimbabwe na nyumbani kwa Rwanda huku Benin ikimaliza ugenini kwa Rwanda na Nigeria.
The post Mokoena aiponza timu ya taifa first appeared on SpotiLEO.