IBRAHIM Bacca beki wa Yanga SC amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Williete SC ya Angola unaotarajiwa kuchezwa leo Septemba 19 2025.
Septemba 18 2025 kikosi cha Yanga SC chini ya Kocha Mkuu, Romain Folz kilifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo wao wakiwa ugenini.
“Kila mchezaji yupo tayari na Wananchi waendelee kutuombea kwa ajili ya mchezo wetu tunamshukuru Mungu temefika salama. Nimekuwa hapa kwenye majukumu yangu na nikipata nafasi nitahakikisha tunapata matokeo mazuri ugenini.
“Kupata nafasi kwenye mechi ambazo tunacheza kwangu ni jambo zuri hasa ukizingatia hii ni kazi yangu. Wachezaji wote tupo tayari na tunapambana kuona kwamba mashabiki wanapata furaha.”
Bacca alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao walianza kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC uliochezwa Uwanja wa Mkapa Septemba 16 2025.
Katika mchezo huo Yanga SC ilipata ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Pacome kiungo mshambuliaji wa Yanga SC.
Wiliete SC ni klabu ya Angola inayopatikana huko Benguela. Ingawa ni klabu changa, imethibitisha kasi ya ukuaji wake kwa kushiriki kwenye ligi kuu ya Angola (Girabola), na kushika nafasi za juu kabisa. Kwa upande wa Yanga SC wanauendea mchezo huu wakiwa ni mojawapo ya klabu kubwa.