BARCELONA: HALMASHAURI ya jiji la Barcelona imekataa kutoa kibali kwa FC Barcelona kurejea katika uwanja wao wa Camp Nou kwa ajili ya mechi ya Jumapili ya LaLiga dhidi ya Real Sociedad kutokana na kile hamlashauri hiyo ilisema ni masuala ya usalama katika uwanja huo unaofanyiwa ukarabati.
Barca walikuwa na matumaini ya kurejea Camp Nou ambako wangepata kibali cha kuingiza watazamaji 27,000 lakini wameshindwa kupata vibali muhimu kutoka kwa Halmashauri hiyo ya Jiji la Barcelona.
Badala yake Barca watakuwa wenyeji wa mechi hiyo kwenye Uwanja wa Lluis Companys Olympic Stadium uliopo katika eneo la Montjuic jijini humo, uwanja ambao walitumia misimu ya 2023/24 na 2024/25 wakati wakisubiri ukarabati wa Camp Nou ambao upo miezi tisa nyuma ya ratiba ya kukamilika kwake.
“Tumekutana na mambo tofauti ambayo yanahitaji kurekebishwa ili eneo lile liwe katika hali ya usalama kwa watazamaji na uwanja,” – alisema mkuu wa ulinzi wa raia Sebastia Massague katika mkutano wa halmashauri ya jiji hilo.
Barca walilazimika kucheza mechi zao za mwanzo za nyumbani kwenye LaLiga katika uwanja wa Estadi Johan Cruyff ambapo mashabiki 6,000 pekee walihudhuria mechi yao dhidi ya Valencia Septemba 14, baada ya tamasha la Post Malone kuacha uwanja wa Lluis Companys katika hali mbaya.
Klabu hiyo imeahidi kufanyia kazi mapendekezo mapya yaliyotolewa na halmashauri hiyo ili kupata ruhusa ya kutumia uwanja wa Camp Nou. Mapema Ijumaa, klabu hiyo ya Kikatalani ilitangaza kuwa mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris St Germain ya Oktoba 1 pia itapigwa Lluis Companys.
The post Barca yakwama tena Camp Nou first appeared on SpotiLEO.