DAR ES SALAAM: KLABU ya mpira wa kikapu ya wanawake ya JKT Stars imetinga hatua ya fainali ya Ligi ya Kikapu ya Wanawake mkoa wa Dar es Salaam (BDL) 2025 baada ya kushinda michezo miwili mfululizo dhidi ya DB Troncatti Girls.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali ulithibitisha uimara wa JKT Stars ambao wameendelea kuonesha ubora wao msimu huu, wakifanikiwa kufika hatua hiyo kwa mara nyingine katika historia ya timu hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Kikapu Dar es Salaam Shendu Mwangala aliipongeza JKT Stars kwa kutinga hatua hiyo akisema ligi hiyo ndio bora kwa sasa nchini.
“Hongera sana JKT Stars kwa kutinga nusu fainali baada ya kushinda michezi miwili, hii ndio ligi bora kwa sasa,”ilisema taarifa ya Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake, Troncatti Girls licha ya kuaga michuano hiyo, wametuma salamu za shukrani kwa mashabiki na wapenzi wao, wakisema wamejifunza mengi na kuibuka na nguvu mpya.
“Tumepoteza nusu fainali lakini tumeshinda heshima, jamii na mustakabali wa baadaye. Safari haijaishia hapa, bali ndiyo msingi wa mafanikio yajayo,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.
JKT Stars wanasubiri mshindi wa mechi kati ya Don Bosco Lioness ambao ndio mabingwa watetezi na Jeshi Stars.
Don Bosco ilishinda mchezo mmoja tayari mwingine itacheza leo usiku kujua nafasi yao ya kusonga mbele.
The post JKT Stars yatinga fainali kikapu Dar first appeared on SpotiLEO.