Beki mpya wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, amefunguka kuwa ni kweli kuna ushindani mkali wa namba kati yake na Chadrack Boka, lakini pia akieleza hadhani kama atakuwa anaanzia benchi mechi zote kwani kuna mashindano mengi sana mbele yao.
Tshabalala, aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Simba, amebainisha kuwa kwenye kikosi chote cha Yanga kuna ushindano mkali wa namba kwenye idara zote na si eneo analocheza yeye, hivyo Kocha Mkuu, Romain Folz, ndiye atakayekuwa akiamua nani anaanza na nani aingie baadaye.
Beki huyo wa kushoto, alisema hayo kutokana na kuonekana akianzia benchi kwenye mechi tatu ambazo Yanga imecheza mpaka sasa.
“Mwalimu ndiye atakuwa anachagua nani aanze nani amalize, timu hii imekamilika kila idara, ina wachezaji bora zaidi ya mmoja na yeyote anayeanza timu inapata ushindi.
“Kwa maana hiyo ni kwamba kweli kuna ushindani wa namba, lakini si kila siku atakayeanza basi atakuwa anaanza mechi zote, mashindano yako mengi sana, naamini kila mtu atapata nafasi ya kuanza na kucheza mechi nyingi kadri iwezekanavyo,” alisema beki huyo wa kushoto ambaye pia huichezea Timu ya Taifa Stars.
Katika mechi ya kilele cha Wiki ya Mwananchi dhidi ya Bandari ya Kenya, Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na mchezo wa kwanza hatua za awali, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete de Benguela ya Angola, mchezaji huyo ambaye pia hutumia jina la Zimbwe Jr, zote hizo aliingia kipindi cha pili kama mchezaji wa akiba, hivyo kuzua minong’ono kwa baadhi ya mashabiki kuwa amekuwa mchezaji wa akiba, badala ya kuanza michezo yote kama alivyokuwa Simba.