MADRID: MSHAMBULIAJI Atletico Madrid Julian Alvarez amegeuka mwokozi wa kikosi hicho baada ya kufunga mabao mawili ndani ya dakika nane za mwisho, kukamilisha hat-trick na kuipa Atletico Madrid ushindi wa 3-2 wa LaLiga dhidi ya Rayo Vallecano kwenye Uwanja wa nyumbani wa Air Riyadh Metropolitano jana usiku.
Ushujaa wa mshambuliaji huyo raia wa Argentina uliokoa kile kilichoonekana kama usiku mwingine wa ndoto mbaya kwa kikosi cha Diego Simeone, ambao ni kama walikuwa wameubali matokeo kabla ya bao la ushindi la Alvarez dakika ya 88.
Atletico walitawala mapema mchezo huo na kupata bao la kuongoza kupitia kwa Alvarez dakika ya 15, bao lililotokana na krosi ya Marcos Llorente iliyomkuta akiwa nyuma ya safu ya ulinzi kisha kuweka mpira kimiani.
Licha ya kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, wenyeji hao walishindwa kutumia nafasi nyingi, ikiwa ni pamoja na ile aliyokosa Alvarez iliyotokana na krosi ya Antoine Griezmann.
Uzembe wao mbele ya lango uliwagharimu pale beki wa kushoto wa Rayo Pep Chavarria alipofunga bao zuri la kusawazisha la umbali wa mita 30 kutoka kwenye lango la Atletico katika dakika za nyongeza za kukamilisha kipindi cha kwanza.
Wageni hao walirejea kwa kasi na nguvu mpya kipindi cha pili, lakini ni Atletico ambao waliendelea kupoteza nafasi nyingi. Rayo waliwaduwaza tena mnamo dakika ya 77 kwa bao la kiufundi la Alvaro Garcia ambalo awali lilikataliwa kutokana na offside kabla ya kuruhusiwa baada ya mapitio ya VAR.
Alvarez ndiye alikuwa msemaji wa mwisho wa mechi hiyo aliposawazisha dakika ya 80 kisha kufunga la ushindi dakika nane baadaye.
Ushindi huu ni wa pili kwa Atletico madrid walioanza msimu kwa kuchechemea wakiwa katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa LaLiga na pointi 9, pointi tisa nyuma ya vinara wa ligi hiyo Real Madrid watakaowatembelea Jumamosi kwenye Dabi ya Madrid.
The post Alvarez awa ‘masia’ wa Atletico Madrid first appeared on SpotiLEO.