DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa Yanga SC, Maxi Nzengeli amesema ni wajibu wa kila mchezaji ndani ya kikosi hicho chini ya sapoti ya mashabiki kuhakikisha timu inaendelea kufanya vizuri na kutwaa mataji mbalimbali msimu huu.
Akizungumza Dar es Salaam baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam amesema wanachezaji wana jukumu la kupambania matokeo na mashabiki waendelee kuwasapoti.
Katika ushindi huo, Nzengeli alikuwa miongoni mwa wafungaji akipachika bao moja, huku mengine yakifungwa na Mudathir Yahya pamoja na Alassane Kouma.
Nzengeli alisema Yanga tayari imeweka historia ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo na jukumu lao ni kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea.
“Sisi tulishashinda ligi mara nne mfululizo, ni jukumu letu kuendelea kuipambania timu kupata mataji. Wananchi waendelee kuisapoti timu kwa kuwa ni muhimu kuliko chochote. Sisi wote tutaifanya timu iendelee vizuri,” alisema Nzengeli.
Aidha, Nzengeli hakusita kumshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa mafanikio aliyopata binafsi, ikiwemo tuzo aliyopewa kutokana na mchango wake.
“Nashukuru Mungu kwa sababu nimepata tuzo, ni jambo zuri kwangu na pia nawapongeza wenzangu wachezaji kwa msaada wao,” aliongeza.
The post Nzengeli: Ni jukumu letu kuipeleka Yanga kileleni first appeared on SpotiLEO.