BARCELONA: MABINGWA wa zamani wa LaLiga Real Madrid watakuwa na jukumu la kuamka kutoka kwenye ndoto mbaya ya kipigo kizito cha Dabi wikiendi iliyopita, itakapowakaribisha Villarreal katika dimba la Santiago Bernabéu, Jumamosi kwenye Ligi Kuu ya Hispania LaLiga.
Kikosi cha Xabi Alonso kilipata kipigo cha udhalilishaji cha mabao 5-2 kutoka kwa mahasimu wao wa jiji Atlético Madrid, matokeo yaliyokuwa ya kwanza kwa wapinzani hao kufunga mara tano kwenye dabi ndani ya kipindi cha miaka 75.
Kipigo hicho kimekuwa fursa kwa FC Barcelona kupaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, ikiongoza kwa pengo la pointi moja dhidi ya Madrid, huku Villarreal ikiwafuata kwa karibu wakiwa pointi mbili nyuma katika nafasi ya tatu.
Madrid, hata hivyo, huenda ikawa iliamka mapema Katikati ya wiki kwa ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Kairat Almaty ya Kazakhstan kwenye Ligi ya Mabingwa, ambapo Kylian Mbappé alifunga hat-trick na kufikisha jumla ya mabao 13 msimu huu.
Kwa upande mwingine, Villarreal ya kocha Marcelino García Toral inaelekea Bernabéu ikiwa na hasira baada ya kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Juventus Jumatano. Zaidi ya hapo, ‘Yellow Submarine’ ina ushindi wa michezo mitatu mfululizo kwenye La Liga, hali inayoongeza mvuto wa mtanange huu.
The post Madrid yajipanga upya kwa Villarreal first appeared on SpotiLEO.