Mchezaji wa timu ya Yanga Princess, Janine Mukandayisenga, ameibuka na kutoa kauli nzito kufuatia hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumsimamisha kushiriki michezo ya ligi ya wanawake hadi uchunguzi wa jinsia yake utakapokamilika. Hatua hiyo imekuja baada ya timu pinzani kuwasilisha ombi rasmi kwa TFF, wakidai kuwa huenda Mukandayisenga si mwanamke halisi kama inavyodaiwa.
Taarifa kuhusu kufungiwa kwa nyota huyo zilianza kusambaa jana katika mitandao ya kijamii, zikieleza kwamba TFF imeona ni muhimu kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli kabla ya kumruhusu kurejea uwanjani. Mchezaji huyo amekuwa tegemeo kubwa kwa kikosi cha Yanga Princess kutokana na uwezo wake mkubwa uwanjani, hali iliyosababisha baadhi ya wapinzani kumtuhumu kuwa ana jinsia ya kiume.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kufungiwa, Mukandayisenga amefunguka na kueleza kuwa anachokiona kinachoendelea ni siasa za mpira ambazo zina lengo la kumvunja moyo. Amesema hana shaka kuhusu jinsia yake kwani yeye ni mwanamke halisi, na wapinzani wanachokifanya ni kwa sababu wanatambua uwezo wake na kuogopa kwamba ataendelea kuwadhuru wanapokutana uwanjani.
“Mimi ni mwanamke na nimekuwa nikicheza soka la wanawake muda mrefu. Hizi ni siasa tu za mpira, najua wanachokifanya kwa sababu wanaogopa nitawafunga,” alisema Mukandayisenga kwa msisitizo.
Hata hivyo, TFF imesisitiza kwamba mchakato wa uchunguzi utaendelea kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote. Mpaka uchunguzi huo utakapo kamilika, Mukandayisenga atasalia nje ya michezo rasmi ya ligi.
Tukio hili limezua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini, huku baadhi wakiiunga mkono hatua ya TFF kama njia ya kulinda uhalali wa mashindano, na wengine wakiliona kama njama ya kumdhoofisha mmoja wa wachezaji bora wa ligi ya wanawake Tanzania. Mashabiki sasa wanasubiri matokeo ya uchunguzi huo yatakayotoa mwanga juu ya hatma ya nyota huyo uwanjani.