ZANZIBAR:TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inatarajia kushuka dimbani leo saa 4:00 usiku kuivaa Zambia katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi utakaopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mchezo huu unatajwa kuwa wa heshima na matumaini, huku Stars ikihitaji ushindi ili kuweka hai ndoto ya kufuzu kama mshindwa bora.
Ikumbukwe kuwa katika mchezo wa mwisho dhidi ya Zambia, Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0, jambo linaloipa matumaini kikosi cha kocha Hemed Morocco.
Mchezaji wa Stars, Bakari Mwamnyeto, amesema bado wana nafasi ya kufuzu na amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao.
“Hatujafuzu bado, lakini tuna nafasi kama mshindwa bora. Watu waje kwa wingi kutusapoti. Kwa asilimia 100, Watanzania ni wale wale – tuwaone leo,” alisema Mwamnyeto kwa msisitizo.
Ameongeza kuwa mchezo huo ni sawa na fainali kwao: “Ni kama fainali. Changamoto yetu kubwa ni kupata pointi tatu. Tumekaa wenyewe tumeongea, tumejiandaa. Tunaamini tunaweza.”
Kwa upande wake Kocha Mkuu Hemed Morocco amesema wachezaji wote wako vizuri kimwili na kiakili kuelekea mchezo huo mgumu.
“Kila mara Tanzania ikikutana na Zambia huwa ni mechi ngumu. Lakini aina ya wachezaji tulionao kwa sasa, tunaweza kushindana. Tukitumia vizuri nafasi tutakazopata, tunaweza kushinda. Hii ni kazi yetu,” alisema Morocco.
Stars inashika nafasi ya pili kwenye Kundi E ikiwa na pointi 10 huku Zambia ikishika nafasi ya nne kwa pointi sita. Kinara ni Morocco yenye pointi 21 na tayari imeshafuzu, Niger ya tatu kwa pointi tis ana Congo ikiwa na pointi moja.
The post Mwamnyeto: Stars, Zambia ni Jasho au Damu first appeared on SpotiLEO.