HATMA ya Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, kuendelea na kibarua cha kuinoa timu hiyo au la itajulikana leo baada ya uongozi wa klabu hiyo kutoa matokeo ya tathimini iliyofanywa kuhusu benchi la ufundi.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, jana alisema uongozi chini ya Kamati ya Utendaji, umemaliza kufanya tathmini hivyo wakati wowote kuanzia leo wanatarajia kutangaza matokeo yake pamoja na kufanya maboresho kidogo.
Uongozi wa Yanga ulifanya tathmini hiyo kutokana na mlalamiko ya baadhi ya wanachama na mashabiki kuhusu kiwango cha timu yao, ingawa timu imekuwa ikipata matokeo mazuri.
Baadhi wanadai timu haichezi soka la kuvutia kama ilivyokuwa misimu mitatu iliyopita, hivyo kutokuwa na imani na kocha Folz, ambaye ameichukua timu hiyo kutoka kwa Miloud Hamdi, aliyetimkia, Ismailia ya Misri.
“Hapa kati kumekuwa na maneno mengi kuhusu kiwango cha timu, mara ya mwisho hivi karibuni nilieleza kwa wanachama na mashabiki kwamba kuna tathmini ambayo uongozi wa klabu inaufanya, niliwaahidi baada ya kufanyika nitarudi kuwaleza ni nini viongozi wamekiamua.
“Niko hapa kuwaambia wanachana na mashabiki kuwa tathmini imekamilika, yako maboresho kidogo ambayo yamefanywa kwenye benchi la ufundi kwa hiyo wakati wowote kuanzia sasa tunaweza kuwatangazia, tunaweka utaratibu sawa tu, lakini kila kitu kimeshakamilika,” alisema.
Aliwataka wanachana na mashabiki kuwa tayari kupokea taarifa ya tathmini pamoja na maboresho hayo kwa manuafaa ya timu yao pamoja na kuyaunga mkono.
“Kwa maana hiyo wanachama na mashabiki wa Yanga wawe tayari na taarifa tutakayoitoa, waone ni kitu gani ambacho uongozi wao umekifanya na maboresho gani yamefanyika,” alisema.
Siku chache zilizopita, Kamwe, alibainisha kuwapo kwa tathimini iliyoanzishwa na viongozi, lakini akadai inafanywa kwenye idara zote ikiwamo yao pia.
“Tathimini inafanyika, lakini siifanyi mimi, inafanywa na Kamati ya Utendaji kwa kushirikiana na idara mbalimbali na hiyo si ya kocha tu au benchi la ufundi, ni ya taasisi nzima inayokwenda kwenye idara mbalimbali, ikiwamo hii ya habari na mashindano ya wanachama,” alisema Kamwe wakati kamati hiyo ilipokuwa inaendelea na tathimini hiyo.
Wakati hayo yakiendelea kikosi cha timu hiyo jana kimeingia kambini rasmi kujiandaa na mchezo wa mkondo wa kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, raundi ya kwanza dhidi ya Silver Strikers ya Malawi.
Habari zinasema kabla ya hapo wachezaji walikuwa wanafanya mazoezi na kurudi nyumbani, ikiwamo mchezo wa kirafiki dhidi ya TRA United, uliochezea katikati ya wiki iliyopita, Uwanja wa Gymkhana, Dar es salaam na kutoka suluhu.
Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa, Jumamosi ijayo, saa 10:00 jioni, Uwanja wa Bingu Mutharika, Lilongwe nchini Malawi.
Kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuondoka wakati wowote kuanzia kesho, huku zaidi ya mabasi 20 ya mashabiki yakitarajiwa kuondoka kwa njia ya barabara kuifuata timu hiyo kwa ajili ya kuipa sapoti.
“Niwapongeze wanachana na mashabiki wa Yanga wa Mbeya na Iringa, wameonekana kuhamasika zaidi kwenda nchini Malawi.
“Dar es Salaam nao naona mwamko umeanza kuwa mkubwa, watu waendelee kujitokeza kwa ajili ya safari,” alisema Kamwe.
The post MAMBO YA FOLZ HUKO YANGA MHHHH…..ALI KAMWE ‘ACHANA JAMVI’ MAPEMA…. appeared first on Soka La Bongo.