MSIMU uliopita wa mashindano 2024/25, Pacome Zouzoua aliwafanya mashabiki wa Yanga kutembea vifua mbele kwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA huku wakicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo, jina lake lilikuwa likiimbwa kila kona.
Huku akifunga mabao 11 na kutoa asisti tisa kwenye ligi, hivyo kuhusika katika mabao 20 kati ya 83 ambayo Yanga ilifunga, ni sawa na kusema alichangia kwa asilimia 24, alikuwa akishindanishwa na Charles Jean Ahoua wa Simba ambaye aliibuka mfungaji bora kwa mabao 16 na asisti tisa katika mjadala wa mchezaji bora wa msimu lakini hata hivyo hapakuwa na sherehe hizo.
Wakati Ahoua akionekana kuanza msimu kwa kupoa, nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ni kama ameanzia alipoishia msimu uliopita kwa kuifanya Yanga kuanza msimu kwa Ngao ya Jamii kutokana na bao alilolifunga dhidi ya Simba, Septemba 16 2025, kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Bao lake lilitonesha kidonda cha wekundu hao wa Msimbazi ambao walichapwa nje ndani msimu uliopita kwa jumla ya mabao 3-0, mechi ya kwanza ilikuwa kwa bao 1-0 huku ya marudiano ikiwa kwa mabao 2-0 wakiwa chini ya Fadlu Davids.
Katika mechi tisa ambazo Yanga imecheza za mashindano yote msimu huu, Pacome amefunga mabao manne na kutoa asisti mbili, mbali na bao la Ngao ya Jamii, mawili amefunga katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete ya Angola na Silver Strikers ya Malawi.
Ilikuwaje? Yanga ilianza safari yake kimataifa huko Angola kwa kucheza dhidi ya Wiliete inayonolewa na kocha wa zamani wa Azam, Bruno Ferry licha ya kwamba hakufunga katika mechi hiyo ya kwanza waliyoibuka na ushindi wa mabao 3-0, alikuwa mwiba katika mechi ya marudiano na kufunga bao moja wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-0.
Katika hatua ya pili, Yanga ilijikuta ikianza vibaya mechi ya mkondo wa kwanza huko Malawi kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers, mechi hiyo ilifanya mabosi wa timu hiyo kuachana na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Romain Folz kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Yanga ikiwa na kazi ya kufanya katika mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam, Pacome aliibuka tena na kuonyesha utofauti kwa kupachika bao la pili dakika ya 34 baada ya Dickson Job kufunga na kuongoza dakika ya sita na kuifanya timu hiyo ya Wananchi kutinga hatua ya makundi kwa mara ya tatu mfululizo.
Mbali na mechi hizo za awali, Pacome ameonyesha pia makali yake katika mechi nne za ligi ambazo Yanga imecheza na kuvuna pointi 10 zilizoifanya kuongoza msimamo huku ikiwa mbele kwa mechi moja dhidi ya Simba yenye pointi tisa.
Katika mechi hizo, Pacome amefunga bao moja na kutoa asisti mbili, bao hilo lilikuwa katika mechi ya mwisho kwa Yanga dhidi ya KMC wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 4-1 kabla ya kalenda ya FIFA pia katika mechi hiyo ambayo aliibuka mchezaji bora alitoa pia kwa Max Nzengeli aliyefunga bao la kwanza kwa Yanga kwenye Uwanja huo wa KMC Complex.
Licha ya kwamba hakufunga katika mechi ya kwanza ya ligi kwa Yanga dhidi ya Pamba Jiji, Pacome alitoa asisti moja na kuisaidia timu hiyo ambayo kwa sasa inanolewa na Kocha Mreno, Pedro Goncalves na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Pamoja na kwamba ndiyo kwanza msimu wa 2025/26 umeanza, Pacome ameonekana kuanza kwa neema kutokana na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, kuitwa na kucheza timu ya taifa la Ivory Coast.
Fundi huyo, aliweka rekodi hiyo, Oktoba 10, 2025 wakati Ivory Coast ikiibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Seychelles huku akicheza kwa dakika zote 90 na kuwa sehemu ya historia kwani ushindi huo uliifanya Ivory Coast kujikatia tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani, 2026 ambazo zinaandaliwa kwa ushirikiano wa mataifa matatu, Marekani, Canada na Mexico.
KIBARUA KILICHOPO
Pacome na wachezaji wenzake wa Yanga, wanakibarua kizito msimu huu, moja kutetea mataji yao ya ndani, pia kufanya vizuri katika hatua ya makundi ambayo msimu uliopita walichemka kwa kushindwa kuvuka hatua hiyo.
Yanga ikiwa chini ya Sead Ramovic ambaye kwa sasa yupo CR Belouizdad ya Algeria msimu ulichemka kutinga robo fainali ya michuano hiyo baada ya kumaliza hatua ya makundi (A) ikiwa nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu, moja pungufu kwa MC Alger walioungana na Al Hilal ya Sudan kusonga mbele.
Licha ya msimu huu, kupangwa kwenye moja ya makundi magumu (B), sambamba na Al Ahly, AS FAR na JS Kabylie, ina nafasi ya kufanya maajabu kutokana na uzoefu wa wachezaji wao katika michuano hiyo, ikumbukwe hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Yanga kutinga hatua ya makundi.
The post MHHHHH…..PACOME HUYU NI YULE YULE AISEEE…. appeared first on Soka La Bongo.





