DAR ES SALAAM: KOCHA wa Simba Queens Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema soka la wanawake limebadilika siku hizi hakuna timu ya kudharau kila mpinzani wanamuheshimu na kuuchukulia mchezo kama fainali.
Kauli yake inakuja baada ya kutoka kushinda mabao 3-0 dhidi ya Bunda Queens katika mchezo wa Ligi Kuu Wanawake uliochezwa jana kwenye Uwanja wa KMC.
Mgosi alisema wanajua ubora wa Bunda Queens na kwa hivyo, walijiandaa vizuri kuwakabili na bahati nzuri walifanya makosa na wao wakawadhibu.
“Bunda ni timu nzuri inajua kucheza kwa kuzuia, ushindani umekuwa ni mzuri kutoka kwao, lakini wamefanya makosa tumewaadhibu. Kwetu sisi tulichukulia kama fainali na kupata kile tunachotaka,”alisema.
Mgosi aliwapongeza wachezaji kwa kiwango walichokionesha akisema wamejipanga kila mchezo kuhakikisha wanachukua pointi tatu ili kufikia malengo waliyojiwekea ya kutwaa taji la Ligi Kuu.
Kocha wa Bunda Quuens, Alley Ibrahim amesema kilichowagharimu ni kuwakosa wachezaji wao muhimu 11 ambao wanne wanafanya mitihani ya kidato cha nne na wengine hajawapata leseni.
Alisema wamefanya makosa na kuadhibiwa na watu ambao ni wakubwa ila wanajipanga kwa kurudi uwanja wa mazoezi wakiwa imara.
The post ‘Kila mchezo kwetu Simba Queens ni fainali’ first appeared on SpotiLEO.




