LEVERKUSEN: WINGA wa Bayer Leverkusen Alex Grimaldo aliinusuru klabu hiyo na kichapo cha nyumbani baada ya kufunga bao la dakika ya 88 lililoiwezesha klabu hiyo kuambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Newcastle United kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano usiku.
Newcastle, ambao pia waligonga mwamba mara mbili, walidhani wamechukua pointi tatu baada ya kutoka nyuma na kuongoza kwa mabao 2-1 kupitia mabao ya Anthony Gordon na chipukizi Lewis Miley, kabla ya Grimaldo kuingia kwa kasi ndani ya boksi na kusawazisha zikiwa zimesalia dakika mbili.
Kwa matokeo hayo, yameiweka Newcastle nafasi ya 12 na pointi 10, huku Leverkusen wakishuka hadi nafasi ya 20 wakiwa na pointi 9. Timu nane za juu hupenya moja kwa moja hatua ya mtoano, zilizopo nafasi ya 9 hadi 24 hucheza playoff kuwania kufuzu hatua ya 16 bora.

“Kwa kweli sijui mchezo ulituponyoka vipi, lakini linatokea mara nyingi sana. Dakika 30 za kwanza tulikuwa vibaya sana, lakini tulijibu vizuri kipindi cha pili. Kocha alitupa msukumo mkali na tukabadilika.” – alisema Gordon, aliyekuwa mchezaji bora wa mchezo.
“Kwa upande wa ulinzi tunahitaji kuwa imara zaidi kwa sababu tunaruhusu mabao ya mwishomwisho kwa kiasi kikubwa, Sijui kama ni uchovu, lakini yote yanakuja kwenye umakini na uimara wa kisaikolojia. Timu kubwa hujua kushikilia matokeo.” – aliongeza.
Leverkusen walitangulia dakika ya 13 baada ya Robert Andrich kuupiga mpira kwa kichwa kwenye ‘far post’ kisha kumgonga nahodha wa Newcastle, Bruno Guimarães, na kuingia wavuni kama bao la kujifunga.

Newcastle walisawazisha dakika ya 51 kupitia penalti ya Gordon baada ya kipa Mark Flekken kuchelewa kuuondoa mpira na kuruhusu Nick Woltemade kuuiba na kuangushwa ndani ya eneo la Hatari.
The Magpies waliendelea kushambulia kwa kasi, Gordon akipiga mwamba kwa shuti kali dakika ya 63 kabla ya kutoa krosi safi iliyomkuta Miley, aliyezamisha bao lake la kwanza kabisa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dakika ya 74.
Newcastle waliendelea kutafuta bao la tatu, Flekken akifanya tajiriba muhimu kuzuia kichwa cha karibu cha Malick Thiaw, kisha shuti la Jacob Murphy kugonga mwamba tena.
Lakini hatimaye ilikuwa Leverkusen waliopata jawabu, Grimaldo akipenya na kufunga kwa mara ya pili mfululizo katika michuano hii, na kuwapa wenyeji pointi muhimu katika dakika za lala salama.
The post Leverkusen yanusurika kwa Newcastle first appeared on SpotiLEO.







