UONGOZI wa Simba umefanya kikao maalum cha kimkakati kwa lengo la kuboresha kikosi chao na kurejesha makali ya timu kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
Taarifa kutoka ndani ya mkutano huo zinasema Bodi ya Wakurugenzi Simba ilikutana kujadili kwa undani mwenendo wa timu katika mashindano yote, ikiwemo tathmini ya matokeo na kiwango cha jumla cha kikosi msimu huu.
Katika kikao hicho, ajenda kubwa ilikuwa ni ujio wa kocha mpya, ambapo imeelezwa kuwa uongozi unahitaji kupata kocha sahihi kabla ya kikosi kurejea kambini ili kuanza maandalizi mapya. Vyanzo vimedai kuwa tayari mchakato wa kumpata kocha huyo umefikia hatua nzuri.
Aidha, kikao hicho pia kilizama kwenye suala la bajeti ya dirisha dogo la usajili, kwa lengo la kuongeza nguvu kwenye maeneo yenye mapungufu ndani ya timu. Inaelezwa kuwa uongozi uko tayari kufanya maboresho makubwa ili kuleta ushindani zaidi.
Mtoa habari kutoka klabuni hapo amethibitisha kuwa uongozi umeafikiana kumpa nafasi kocha mpya atakayekuja kuungana na benchi la ufundi lililopo sasa, huku Seleman Matola akiendelea na majukumu yake kama kocha msaidizi.
“Tunalenga kutumia vyema kipindi hiki cha AFCON kuirudisha timu kwenye uimara wake ili iweze kushindana vema kimataifa na kwenye ligi ya ndani,” kilisema chanzo hicho.
The post SIMBA YAIBUKA NA MIKAKATI YA UBORA MPYA appeared first on Soka La Bongo.






