MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki kinachoendelea ndani ya timu.
Wito huo umetolewa kufuatia kauli ya Rais wa Yanga, Hersi Said, aliyotoa katika kongamano lililoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) mjini Doha, ambapo alitolea mfano klabu ya Simba kuhusu mada ya migogoro ya kiuongozi.
Kauli hiyo ya Hersi imezua hisia kali miongoni mwa mashabiki na wanachama wa Simba, wengi wao wakionyesha kutoridhishwa na klabu yao kutajwa kama mfano mbaya katika jukwaa la kimataifa.
Ahmed amesema hakuna sababu ya mashabiki kuingia katika taharuki, akisisitiza kuwa uongozi wa Simba unaendelea kufanya kazi kwa utulivu na umakini mkubwa.
Ameeleza kuwa kwa sasa viongozi wa klabu wapo kwenye mchakato wa kuboresha benchi la ufundi sambamba na kurekebisha baadhi ya mambo muhimu ndani ya timu kwa lengo la kuimarisha ushindani.
“Tuwape viongozi wetu uhuru wa kufanya maamuzi sahihi kwa kuzingatia mahitaji ya timu pamoja na maoni chanya yanayotolewa na mashabiki,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa utulivu na subira ni nguzo muhimu za maendeleo ya taasisi yoyote, hivyo Wanasimba hawana budi kutumia silaha hizo katika ujenzi na uimarishaji wa klabu yao.
The post AHMEDY ALLY AWATULIZA WANA MSIMBAZI appeared first on Soka La Bongo.






