Nyota wawili wa Simba SC, Jonathan Sowah na Allasane Kanté, wamekutana na adhabu kali ya kufungiwa michezo mitano kila mmoja pamoja na kutozwa faini ya Sh milioni 1,000,000.
Adhabu hiyo imetangazwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya kubaini ukiukwaji wa kanuni uliojitokeza katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, tukio lililovuta hisia kubwa miongoni mwa wadau wa soka.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, Sowah ameadhibiwa kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji Himid Mao, huku Kanté akipewa adhabu kwa kumpiga teke kwa makusudi Feisal Salum wa Azam FC.
TPLB imesema adhabu hizo zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji, inayolenga kuhakikisha heshima, usalama na nidhamu vinazingatiwa uwanjani.
“Adhabu hizi zinatolewa ili kutuma ujumbe wazi kwamba vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira wa miguu havikubaliki na vitachukuliwa kwa uzito unaostahili,” ilieleza taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu.
Kutokana na adhabu hiyo, Sowah na Kanté watakosa mechi tano zijazo za Simba dhidi ya Mtibwa Sugar (nyumbani), Singida Black Stars, KMC FC, TRA United (nyumbani) na Tanzania Prisons, mechi ambazo nyingi zitachezwa ugenini.
Katika hatua nyingine, mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano baada ya kubainika kushindwa kutafsiri sheria ipasavyo na kuchukua hatua stahiki dhidi ya makosa ya Sowah na Kanté.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi, ikisisitiza wajibu wa waamuzi kusimamia haki na nidhamu katika mechi zote za ligi.
The post NYOTA WA SIMBA KUSUGUA BENCHI NJE YA DIMBA appeared first on Soka La Bongo.







