UONGOZI wa Klabu ya Simba umeweka wazi kuwa baada ya kikosi kurejea kambini, kutakuwa na mazungumzo ya kina kati ya benchi la uongozi na wachezaji wote kwa lengo la kuwakumbusha misingi muhimu ya nidhamu na uwajibikaji ndani na nje ya uwanja.
Hatua hiyo imekuja kufuatia adhabu ya kufungiwa michezo mitano kwa nyota wawili wa klabu hiyo, Jonathan Sowah na Allasane Kante, hali iliyosababisha pigo kwa kikosi cha Simba katika kipindi hiki cha ushindani mkali wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kukosekana kwa Sowah na Kante kwa michezo mitano ni hasara kubwa kwa timu kutokana na mchango na umuhimu wao ndani ya kikosi.
Ahmed amesema uongozi wa klabu umepokea adhabu hiyo na uko tayari kuitumikia kwa mujibu wa kanuni, lakini umeona kuna ulazima wa kufanya kikao cha pamoja na wachezaji wote ili kuwajenga kisaikolojia na kuwakumbusha wajibu wao wa kulinda maslahi ya klabu.
Ameeleza kuwa adhabu kama hizo haziwaumizi wachezaji binafsi pekee, bali huathiri klabu kwa ujumla, hasa inapobidi kukosa huduma ya wachezaji muhimu katika ratiba ndefu na yenye ushindani mkubwa.
“Kwa sababu mwisho wa siku wanaoathirika ni sisi kama klabu. Unapofungiwa mechi tano kati ya 30 za Ligi Kuu, unakuwa umecheza mechi 25 tu, ukizingatia pia uwepo wa kadi za njano na majeruhi. Ndiyo maana tunasisitiza nidhamu na kuzingatia misingi ya kazi,” amesema Ahmed.
The post SOWA, KONTEAWAPONZA WENZAKE SIMBA appeared first on Soka La Bongo.








