UONGOZI wa Klabu ya Simba umehitimisha mchakato wa kumpata kocha mkuu mpya ambaye anatarajiwa kutambulishwa rasmi hivi karibuni kabla ya kuanza majukumu yake ndani ya kikosi hicho chenye malengo makubwa msimu huu.
Imeelezwa kuwa kocha huyo atajiunga na timu mara itakaporejea kambini Desemba 28 kwa ajili ya kujiandaa na mashindano yaliyopo mbele yao, yakiwemo ya Kombe la Mapinduzi linalotarajiwa kuanza Desemba 29, 2025 hadi Januari 13, 2026.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally, amesema mchakato wa kumpata kocha huyo umefikia hatua nzuri, huku akibainisha kuwa dalili za mafanikio tayari zinaonekana na muda si mrefu mashabiki watapata taarifa kamili.
Ahmed amesema uongozi wa klabu umeamua kuwa kimya kwa muda ili kumpata mtu sahihi, akisisitiza kuwa walikuwa wakitazama kwa umakini aina ya kocha anayefaa kulingana na malengo ya klabu na mahitaji ya msimu huu.
Ameongeza kuwa Simba inahitaji mwalimu mwenye uwezo wa kuisogeza timu mbele kutoka ilipo sasa, ndiyo maana tathmini ya kina ilifanywa na viongozi wa juu wa klabu bila kufanya maamuzi ya haraka.
“Mwalimu ambaye anaweza kutuvusha hapa tulipo ndiye tuliyekuwa tunamtafuta. Tumejifungia kufanya tathmini ya kina ili kumpata mtu sahihi na bila shaka tayari tumeshampata, kilichobaki ni kumtangaza rasmi,” amesema Ahmed.
The post KOCHA MPYA SIMBA KUANZA NA MAPINDUZI appeared first on Soka La Bongo.








