DOHA: SHIRIKISHO la Soka Ulaya (UEFA) limetangaza kuwa Mabingwa wa Ulaya, timu ya Taifa ya Hispania watakutana na mabingwa wa Copa America timu ya Taifa ya Argentina katika mchezo wa ‘Finalissima’ utakaochezwa nchini Qatar mwezi Machi mwaka ujao.
Mchezo huo unaowakutanisha mabingwa wa mabara mawili ulirejeshwa mwaka 2021 baada ya UEFA na Shirikisho la Soka Amerika Kusini (CONMEBOL) kupinga vikali mpango wa FIFA wa kuanzisha Kombe la Dunia linalochezwa kila baada ya miaka miwili.
Argentina chini ya Lionel Messi iliitandika Italia mabao 3-0 katika Finalissima ya mwaka 2022, na sasa itarejea katika Uwanja wa Lusail, ambako ilitwaa Kombe la Dunia miaka mitatu iliyopita.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa Machi 27, 2026, na utaanza saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki
Hispania na Argentina zimekutana mara 14 katika historia yao, kila timu ikishinda mechi sita, huku michezo miwili ikimalizika kwa sare.
The post Ni Messi Vs Yamal ‘Finalissima’ 2026 first appeared on SpotiLEO.








