*Yasema imenzisha skimu maalumu kwa ajili waliojiajiri wenyewe pamoja na walioajiriwa lakini wanapenda kujiwekea akiba
Na MWANDISHI WETU,
Dodoma.
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewataka Watanzania kujenga
utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kujiunga na kuchangia NSSF ili waweze
kujikinga na majanga kama vile uzee na ukosefu wa kipato kwa kunufaika
na mafao yanayotolewa na Mfuko.
Aidha, NSSF imesema imenzisha
skimu maalumu kwa ajili ya kuwafikia wananchi waliojiajiri wenyewe
wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, mama
lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine ili waweze kujiwekea akiba kwa
ajili ya kesho yao iliyokuwa njema.
Hayo yalisemwa na Meneja wa
NSSF wa sekta isiyo rasmi, Bi. Rehema Chuma, tarehe 20 Novemba 2024
jijini Dodoma kwenye mkutano wa Chama Cha Wahasibu Wanawake Tanzania.
Amesema
NSSF umeanzisha mpango wa kitaifa kwa sekta isiyo rasmi kwa lengo la
kuwafikia watanzania wote waliojiajiri wenyewe ambapo wanaweza kujiwekea
akiba kwa kima cha chini cha shilingi 30,000 ambapo atanufaika na mafao
pamoja na huduma ya matibabu kwa mtu mmoja na atakeyejiwekea akiba ya
52,200 atanufaika na mafao pamoja na huduma za matibabu yeye mwenyewe na
familia yake na kuwa mtu anaweza kuchangia hata shilingi 1000 kwa siku.
Amesema
utaratibu wa kujichangia ni rafiki na rahisi sana ambapo unaweza
kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo na kuwasilisha michango popote
ulipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za Mfuko au kutumia wakala.
“Kujiunga
na skimu hii ni rahisi sana unaweza kutumia simu ya kiganjani kwa
kupiga *152*00# kisha unaenda namba 3, kisha unaenda namba 6 unachagua
NSSF, kisha namba Moja ambapo utaingiza namba ya NIDA na hapo hapo
utakuwa umesajiliwa ambapo pia unaweza kutumia mfumo huo kujilipia
michango yako na kuangalia taarifa nyingine,” amesema Bi. Rehema.
Kuhusu
skimu ya uchangiaji wa ziada, Bi. Rehema asema ni kwa ajili ya
Watanzania walioajiriwa lakini wanapenda kujiwekea akiba kwa hiari ili
kuongeza kipato wakati wa kustaafu.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa
Chama cha Wahasibu Tanzania, Tumaini Lawrence, ametoa wito kwa wahasibu
ba wataalamu wa kada nyingine kuchangamkia fursa ya kujiunga na
kuchangia NSSF kupitia mpango wa ziada (Supplementary Scheme) na wa
sekta isiyo rasmi ili waweze kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho yao
iliyokuwa njema.
“Katika mkutano huu tupo na ndugu zetu wa NSSF
ambao wapo hapa kwa ajili ya kutupa elimu hasa kupitia skimu ya
uchangiaji wa ziada pamoja na ile ya sekta isiyo rasmi ambapo unaweza
kujiwekea akiba hata kama ni mwajiriwa wa Serikali NSSF wanakuruhusu
kujichangia kwa ajili ya kesho iliyokuwa njema,” amesema Bi. Tumaini.
Kwa
upande wake, Bw. John Masatu, Afisa Matekelezo kutoka sekta isiyo rasmi
amesema mwanachama anaweza anaweza kujisajili popote alipo kwa kutumia
simu ya kiganjani na kuwa wataendelea kuwafikia wananchi wengi wengi
zaidi kuwapa elimu ya hifadhi ya jamii na kuwahamasisha kujiunga.