NA MWANDISHI WETU
BENKI
ya NMB imekuwa Taasisi ya Kwanza ya Kitanzania kupata ithibati ya kuwa
Mwajiri Kinara Tanzania kwa Mwaka 2025, inayotolewa na taasisi bobevu na
mahiri ya masuala ya rasilimali watu ya Top Employers Institute ya
Uholanzi, ambayo kwa mwaka huu imetoa vyeti vya uKinara kwa taasisi bora
katika nchi 124 duniani.
Hii
sio mara ya kwanza NMB kutambulika kama Mwajiri Kinara, kwani tayari
imetunukiwa Tuzo ya Mwajiri Bora Tanzania kwa Mwaka 2023 na Chama cha
Waajiri Tanzania (ATE), lakini pia ilipata Tuzo ya Mwajiri Bora Afrika
Mwaka 2022 kutoka Employer Branding Institute, taasisi bobevu ya masuala
ya ajira duniani.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Alhamisi ya Januari 16,
Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay, alisema
ni fahari kwa taasisi yake kuwa miongoni mwa mashirika 2,400 duniani
yaliyotambuliwa na kutunukiwa uthibitisho huo wa uKinara kwa mwaka 2025.
Alibainisha
kuwa, Top Employers Institute ni taasisi kinara duniani katika kufanya
tafiti na ukaguzi huru wa mashirika kuhusu rasilimali watu, ikitumia
vigezo vya kimataifa na wanajivunia tuzo hiyo ambayo inathibitisha kuwa
NMB ni taasisi imara ya ajira na kiongozi katika maendeleo ya rasilimali
watu nchini.
“Tuzo
hii kutoka Top Employers Institute ni muhimu sana kwetu kama mwajiri wa
takribani watu 4,000, kwani wafanyakazi walio tayari kujitolea na wenye
motisha wa kuhudumia, ni msingi wa huduma Kinara na mojawapo ya njia kuu
za kuwaridhisha wateja wetu.
“Uthibitisho
wa Mwajiri Kinara unathibitisha thamani ya juhudi zetu na kuimarisha
shauku yetu ya kuhakikisha kila mtu anafanikiwa.
“Pia,
hii tuzo inayoakisi ahadi yetu ya mazingira Kinara kazini, yenye ustawi
kwa wafanyakazi, ambao wanajivunia na kufurahia ajira zao. Kama sehemu
ya mkakati wetu wa biashara, tunafanya uwekezaji mkubwa wa kuwa na
utamaduni jumuishi ambapo watu wetu wanahisi kuthaminiwa na
kushirikishwa,” alibainisha Akonaay.
Aliongeza
ya kwamba, kuna sababu kadhaa zilizowawezesha kutwaa tuzo hiyo, ikiwemo
kuwa na mikakati bora juu ya wafanyakazi, upatikanaji wa wafanyakazi
bora, uendelezaji wa wafanyakazi, namna bora ya kuwatumia wafanyakazi
kulingana na ubora wao, utofauti na ujumuishaji na ustawi wa
wafanyakazi.
Akonaay
aliongeza kuwa kwa mwaka huu 2025, Taasisi ya Top Employers imetoa vyeti
vya uKinara kwa taasisi mbalimbali katika nchi 124 duniani, ambazo kwa
pamoja zina athari chanya kwenye maisha ya zaidi ya wafanyakazi zaidi
milioni 13 kupitia mbinu Kinara za Rasilimali Watu na Mazingira Kinara
ya Ajira.
“Kutunukiwa
huku kwa Benki ya NMB kumetokana na kushiriki katika utafiti wa ‘Mbinu
Kinara za Rasilimali Watu,’ ulioendeshwa na Top Employers Institute, kwa
kuzingatia viwango vya kimataifa na kuwalinganisha washiriki kwa vigezo
vya mbinu Kinara za ajira zinazotambulika na kutumika duniani.
“Mchakato
wa tathmini ya washiriki ulizingatia maeneo sita muhimu katika masuala
ya rasilimali watu na sehemu 20 za sera na mbinu za utendaji kazi. Hizi
ni pamoja na mkakati wa usimamizi na maendeleo ya wafanyakazi,
upatikanaji na usimamizi wa vipaji, huduma za ustawi, utofauti na
ujumuishwaji, pamoja na kuwa na mazingira rafiki ya kazi.
Alisema
kwamba, tuzo hiyo inaenda kuwa chachu ya NMB kuendelea kuwa bora zaidi,
huku ikiendelea kuboresha utamaduni wake katika ufanyaji kazi na kubuni
mbinu bora za uajiri ili kukidhi mahitaji yanayobadilika ya
wafanyakazi.
“Ulimwengu
wa kazi unabadilika, na NMB tumejikita katika kukabiliana na mabadiliko
haya kwa kuwekeza katika watu wetu na kukuza mazingira yanayochochea
ukuaji, tutahakikisha tunabaki kwenye njia yetu ya ubora na kuifanya
benki kuwa kinara katika huduma za kifedha na hata katika ustawi wa
wafanyakazi wake,” alisisitiza Akonaay.