Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas kushoto na Mkuu wa wilaya ya Songea Kapenjama Ndile katikati,wakimsikiliza Mhifadhi wa msitu asili wa Matogoro Mussa Kitivo kulia kuhusiana na vivutio mbalimbali vilivyopo katika msitu huo.
Baadhi ya Wakazi wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,wakiangalia Bustani ya miti katika safu za milima ya Matogoro ambayo imeoteshwa kwa ajili ya kugawa kwa taasisi za Serikali na Wananchi.
Na Mwandishi Wetu,Ruvuma
JUMLA ya Watanzania 871 na raia 9 kutoka Mataifa ya Kigeni wametembelea msitu wa Hifadhi ya asili Matogoro kata ya Ndilimalitembo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na walioingiza zaidi ya Sh.1,472,390 tangu mwaka wa fedha 2024/2025.
Mhifadhi Msitu wa Mazingira asilia Matogoro Mussa Kitivo,amesema hayo jana alipokuwa anatoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas aliyetembelea msitu huo kwa ajili ya kuona shughuli za uhifadhi na vituo mbalimbali vilivyopo katika msitu wa Matogoro.
Kitivo alisema, kwa mwaka 2023/2024 watalii wa ndani 2,341 na wa nje 30 walitembelea msitu wa Matogoro ambapo Serikali kupitia wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)ilikusanya Sh.5,467,000.
Aidha alieleza kuwa,mwaka 2021/2022 TFS imepokea Sh.394,135,000 za mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya Uvico-19 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha vumbi yenye urefu wa kilometa 9.
Kwa mujibu wa Kitivo,kazi zilizofanyika ni kujenga njia ndogo ya miguu yenye urefu wa kilometa 4.3 pamoja na kuboresha lango kuu la kuingilia katika msitu ili kurahisisha wageni wa ndani na nje kufika kirahisi kwenye msimu huo.
“katika msitu wa hifadhi Matogoro kuna vivutio mbalimbali ikiwemo miinuko mikubwa ambayo imesambaa katika eneo kubwa la msitu inayomwezesha mtu kuona maeneo mengi ya mji wa Songea na vijiji vyake”alisema Kitivo.
Ametaja vivutio vingine,ni chanzo cha mto maarufu na mkubwa wa Ruvuma wenye urefu wa kilometa 800 ambao unamwaga maji yake kwenye Bahari ya Hindi mkoani Mtwara.
Alisema,ndani ya msitu wa Matogoro kuna vyanzo 8 vya maji(Intake) kutoka mito ya Ruvuma,Luhira na Lipasi ambayo ni tegemeo kubwa la maji kwa wakazi Songea na mapango ambayo hutumika kwa ajili ya tiba za jadi na matambiko ya asili kwa watu wa Songea na mikoa jirani.
“katika msitu wa Hifadhi Matogoro tuna wanyama wadogo na wakubwa kama Swala,Digidigi,Ngedere,Nyani,Chui,Nyati na Simba pamoja,ndege,vipepeo pamoja na uoto wa asili,mimea mbalimbali na hali ya hewa ambayo haipatikani eneo lingine ndani ya mkoa wa Ruvuma”alisema Kitivo.
Hata hivyo alisema,mkakati walionao kwa sasa ni kuongeza makusanyo yatokanayo na utalii kwa kutafuta mwekezaji ili kujenga Hoteli ya Kitalii katika eneo ambalo unaweza kuona mji wote wa Songea kutoka milimani(View Point).
Kitivo alitaja mkakati mwingine ni kutangaza na kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje kutoka 2,341 hadi kufikia 5,000 mwaka mwaka huu,kujenga miundombinu ya choo cha kudumu,jiko la kisasa na kuweka vifaa vya michezo kwa watoto katika eneo la pikiniki.
“TFS kwa kushirikiana na wadau tutafanya utafiti wa mwelekeo wa upepo ili kuongeza zao jipya la utalii wa kuruka na Parachuti kutokea view point namba mbili na kutoa huduma ya malazi kwa wageni watakaohitaji kulala ndani ya hifadhi”alisema.
Kwa upande wake Kamanda wa wakala wa huduma za misitu Tanzania kanda ya kusini Manyise Mpokigwa alisema,TFS inasimamia misitu minne inayotumika kama sehemu ya utalii ikiwemo msitu wa asili Matogoro ambako kuna mapango makubwa yaliyotumika wakati wa vita vya Majimaji.
Alisema,Matogoro kuna utalii mpya wa Ikolojia ambao ni zao jipya tofauti na utalii uliozoeleka wa wanyama na msitu wa Mwambesi uliopo wilaya ya Tunduru ambao unatumika kwa utalii wa Ikolojia ambao umeanza kuvutia watu wengi hasa kutoka mataifa ya nje.
Ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma na kanda ya kusini kwa ujumla, kwenda kutembelea misitu ya asili yenye vivutio vingi na maeneo mazuri yanayoweza kutumika kwa ajili ya sherehe za harusi,mikutano na mapumziko.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas,amewapongeza TFS kwa kuwa na maeneo mengi ya vivutio vya utalii katika mkoa wa Ruvuma ambavyo vitahamasisha wageni wa ndani na nje ya nchi kutembelea Ruvuma na kuchangia pato la mkoa na Taifa kwa ujumla.
Abbas,amewomba wananchi kuwa na mazoea ya kutembelea vituo vilivyopo ambavyo ni urithi mkubwa badala ya kuwaangalia watu kutoka nje kutembelea na kunufaika na vivutio hivyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Ndilimalitembo Magnus Nyoni alisema,tangu msitu huo ulipoanzishwa kuwa msitu wa Hifadhi wamefanikiwa kupata ajira mbalimbali na kuuza bidhaa wanazozalisha kwa wageni wanaotembelea msitu huo.