Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bw. Christian Nyakizee akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 6,2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2024.
………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefatilia miradi mitano yenye thamani ya shilingi 2,808,572,120, huku miradi miwili yenye thamani ya shilingi 144,800,000 imebainika kuwa na mapungufu ambapo wahusika wameshauriwa kurekebisha mapungufu hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 6,2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2024, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bw. Christian Nyakizee, amesema kuwa pia katika mradi mmoja wa ujenzi wenye thamani ya shilingi 90,000,000 ulibainika kubadilishwa kazi iliyotolewa kibali cha awali.
Bw. Nyakizee amesema kuwa kibali kilichotolewa kwa ajili ya kufanya ukarabati wa majengo, badala yake wakaanzisha ujenzi wa madarasa mapya jambo ambalo ni kosa la kisheria kubadili matumizi ya fedha bila kibali kutoka sehemu husika, ambapo bado wanaendelea kufatilia kwa kina kuhusu suala hilo.
“Katika kipindi husika tulifanya uchambuzi wa mifumo ili kubaini mianya ya rushwa maeneo ya kiutendaji ya ofisi za taasisi au idara mbalimbali ili kuidhibiti ikiwemo usimamizi na ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekroniki katika Manispaa ya Ubungo na Kinondoni katika uwasilishaji wa michango mifumo ya hifadhi ya jamii” amesema Bw. Nyakizee.
Amesema kuwa katika uchambuzi wa mifumo miongoni mwa maeneo yaliobainika kuna mapungufu ni pamoja na baadhi ya watumishi kutowasilisha fedha za makusanyo katika akaunti ya serikali pamoja na wahasibu wa Halmashauri kutofanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wakusanyaji ushuru.
Bw. Nyakizee amesema kuwa pia wamefanikiwa kupokea malalamiko 85 na kati ya hayo malalamiko 46 yalihusu rushwa, huku 36 hayakuhusu rushwa.
Ameeleza kuwa malalamiko ambayo hayakuhusu rushwa walalamikaji wameshauriwa na majalada kufungwa na wengine wameelekezwa sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko yao.
“Kwa malalamiko yanayohusu vitenda vya rushwa majalada yanaendelea kushughulikiwa na hayo katika hatua mbalimbali za utekelezaji” amesema Bw. Nyakizee.
Amesema kuwa wamefanikiwa kufungua mashauri sita katika Mahakama ya Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo na Jamhuri imeshinda mashauri mawili, huku mashauri 27 yanaendelea mahakamani.
Katika hatua nyengine amesema kuwa katika uchaguzi wa serikali za mtaa 2024 wananchi walipewa elimu kuhusu madhara ya rushwa kipindi cha uchaguzi na kuhamasishwa kushirikiana na TAKUKURU kutokomeza vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Bw. Nyakizee ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU na kuwasihi kutoa taarifa za rushwa kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwa namba ya dharura 113 na kufuata maelekezo au kufika katika ofisi za TAKUKURU iliyopo karibu.