Na Mwandishi wetu, Arumeru
BAADHI ya wakazi wa Kata tatu za Naisinyai Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, Majengo Wilayani Arumeru Mkoani Arusha na Kia Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro, wamefunga barabara kwa muda wa saa tatu kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 2 asubuhi leo jumanne ya Februari 11 mwaka 2024 wakishinikiza kufanyiwa ukarabati wa miundombinu ya mto inayosababisha mafuriko na kufanya washindwe kulima mashambani kwa kukosa mazao baada ya maji kutuama.
Watu hao zaidi ya 1,500 wakiwemo wanawake na wanaume wameandamana na kufunga barabara inayotoka mji mdogo wa Mirerani hadi uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kusababisha magari kushindwa kupita eneo hilo la kona ya punda.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amiry Mkalipa akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo, alifika eneo hilo na kuzungumza na watu hao waliofunga barabara na wapishe barabara na suala hilo litatuliwa na Serikali.
“Ila msirudie tena kufunga barabara kwani mna viongozi wenu madiwani mkimtaka DC hata usiku mwambieni Diwani wenu ana uwezo wa kumwita ana gari, na suala la kuhusisha wanawake kushiriki maandamano na kufunga barabara siyo vizuri pia sheria ya maji yakijaa usivuke yaache yapite,” amesema DC Mkalipa.
Awali, wakazi hao wa kata tatu wakiwa na mabango mbalimbali walifunga barabara hiyo, licha ya kutakiwa na viongozi wao wakiwemo wenyeviti wa vijiji, madiwani, viongozi wa kimila wa jamii ya kifugaji na askari polisi, kupisha barabara hiyo waligoma hadi DC Mkalipa alipowasihi.
Mkazi wa kata ya Majengo Wilaya Arumeru Mkoani Arusha, Elias Mollel amesema wamefunga barabara ili kilio chao kiweze kufikiwa kwani mafuriko yamesababisha vifo, majeruhi na mazao yao kusombwa na maji.
“Maandamano haya yamewasilisha ujumbe wetu kuwa tumezuia barabara kwa amani kwani tunakufa na njaa kutokana na mto huu kutofanyiwa ukarabati ili maji yake yasituletee madhara wakati wa mafuriko,” amesema Mollel.
Mkazi wa kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro, Isack Kitwana amesema zaidi ya miaka mitano wanateseka kutokana na mafuriko hayo kwani hivi karibuni walitembelewa na viongozi na wataalamu ila hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.
“Maji hayo yanatoka kwenye mito mitatu ikiwemo mto Kikuletwa na kukusanyika sehemu moja ila kutokana na kutokuwepo miundombinu inayoweza kusababisha maji hayo ambayo yanakwenda kugota kwenye kingo ya barabara na kusababisha mafuriko,” amesema Kitwana.
Mkazi wa kata ya Kia Petro Laizer amesema mafuriko yanayosababishwa na mto Kikuletwa yameathiri watu wengi kwenye kata hizo hivyo Serikali ichukue hatua.
“Mito mitatu imekutana na mto Kikuletwa na maji yake yameelekezwa kwenye vijiji vitatu nakusababisha mafuriko kwani maji yanakwenda kwenye makazi na mashambani,” amesema Laizer.
DC Mkalipa amewaeleza watu hao kuwa watakutana na wakuu wa wilaya hizo tatu za Arumeriu, Hai na Simanjiro na madiwani wa Kata tatu na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na viongozi wa TANROADS, TARURA, bonde la Pangani na watendaji wa Kata na vijiji, kuhusu utatuzi wa suala hilo ndani ya uwanja wa ndege wa KIA.
“Ili kufikia mwisho wa suala hili inatupasa wote tukubali kupoteza, Serikali itatoa fedha na rasilimali watu na baadhi ya waliopo kando ya mto waache kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 pembeni ya mto Kikuletwa,” amesema DC Mkalipa.