Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, Mhe. Mohamed Ali Nafti pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025 Addis Ababa, Ethiopia.
….
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Tunisia zimejadiliana juu ya kuanzisha Ushirikiano wa Pamoja wa Kiuchumi ili kurasimisha maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa na kuruhusu ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa maeneo husika.
Hayo yamesisitizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, Mhe. Mohamed Ali Nafti pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025 Addis Ababa, Ethiopia.
Pamoja na masuala mengine mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi hususan katika eneo la nishani ya umeme na gesi ambapo Waziri Nafti ameeleza kuwa Tunisia ina kampuni za kimataifa zilizowekeza kwenye sekta ya nishati katika nchi za Afrika hivyo, Tunisia ina nia ya dhati ya kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na hata katika kujenga uwezo wa kitaalamu.
Vilevile, Mhe. Nafti ameeleza kuwa Tunisia inazalisha mafuta ya kupikia kwa wingi hivyo, ipo tayari pia kushirikiana na Tanzania katika eneo hilo ili kujenga uchumi wa pande zote mbili.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Tunisia zimetimiza miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia tangu kuanzisha kwa ushirikiano huo.
Aidha, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuitisha Mkutano wa Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi ambapo pande zote zimeahidi kuleta ujumbe wa wafanyabiashara pembezoni mwa mkutano huo. Mpango huo utawawezesha wafanyabiashara kufahamiana na kunadi fursa mbalimbali zilizopo katika mataifa yao kwa lengo la kujenga mtandao imara wa biashara ya kikanda kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFT) na biashara ya kimataifa.
Pia, Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Tunisia katika kujenga uwezo wa mchezo wa mpira wa miguu nchini ambapo, alieleza kuwa Tunisia imepiga hatua kubwa kwenye uwekezaji wa mpira huo hivyo, ushirikiano huo utasaidia katika masula ya kuanzisha shule za mpira pamoja na kujenga uwezo wa wachezesha mpira ili kuweka mfumo bora wa usimamizi utakaoinua kipato kwa wachezaji na Taifa kwa ujumla.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Tunisia zimetimiza miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia tangu kuanzisha kwa ushirikiano huo.