……………….
Na Sixmund Begashe – Serengeti
Uongozi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti umetakiwa kuongeza nguvu katika ulinzi wa Maliasili kwa kutumia zaidi teknolojia ya kisasa ili kudhibiti matendo ya uhalifu katika Hifadhi hiyo yenye mvuto zaidi Duniani.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba alipokutana na kuzungumza na uongozi wa Hifadhi za Taifa Tanzania ikiwemo Menejimenti ya Hifadhi ya Serengeti iliyopo Mkoani Mara.
CP. Wakulyamba amesema, ulinzi wa Maliasili katika Hifadhi hiyo na zingine hapa nchini siyo jambo la mzaha hata kidogo, hivyo jitihada zaidi zichukuliwe katika kukabiliana na wahalifu wenye nia ovu ya kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika usimamizi wa maliasili hapa nchini.
“Pamoja na kazi nzuri mnayoifanya ya kulinda Maliasili katika Hifadhi hii, hakikisheni mnasimamia vyema nidhamu kwa Askari wa Uhifadhi. Niwajuze tu kwamba, suala la ulinzi wa Maliasili si jambo la mzaha hata kidogo, tusikubali na kuwapa nafasi wavunja sheria wachache kuchezea maliasili zetu kwa manufaa yao binafsi,” alisema CP. Wakulyamba.
Aidha, CP. Wakulyamba ameitaka Menejimenti ya Hifadhi hiyo, kuhakikisha inaendelea kusimamia nidhamu kwa Askari wa Jeshi la Uhifadhi ili kuhakikisha ulinzi endelevu wa Maliasili unakuwepo na kuwa, amewataka viongozi hao kutokusita kumchukulia hatua za kinidhamu na kisheria mtumishi yeyote atakayekiuka taratibu na misingi ya kazi za uhifadhi.
Vilevile, akiwa katika ziara hiyo, ametembelea Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii Ikona (WMA) iliyoko pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti ambapo Kamishna Wakulyamba ameupongeza uongozi wa Jumuia hiyo kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuwapokea na kuwahudumia wageni huku akiwataka viongozi hao kuendelea kushirikiana vyema na Hifadhi ya Taifa Serengeti katika suala zima la uhifadhi kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesisitiza pia kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ili kuepusha madhara kwa binadamu na kuhakikisha wanachukua hatua stahiki na za haraka pale matukio yanapojitokeza katika eneo lao.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania, Naibu Kamishna wa Uhifadhi, anayesimamia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Massana Mwishawa amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa watatekeleza maagizo yote ili kuendelea kuimarisha ulinzi wa Maliasili katika Hifadhi hizo ambazo ni chachu kubwa kwa pato la Taifa.