Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoan Mara, Bw. Msongela Palela, akisoma kipeperushi alichokabidhiwa na Afisa Usimamizi wa Sekta ya Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizaya ya Fedha Bw. Santley Kibakaya, chenye mada kuhusu uwekezaji ikiwa ni moja ya mada ambayo itafunzishwa wakati wa utoaji elimu ya fedha kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Bw. Msongela Palela, akizungumza na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha iliyofika mkoani Mara kwa lengo la kutoa elimu ya fedha katika maeneo mbalimbali mkoani humo. Kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bi. Elizabeth Mzava na kulia ni Afisa Usimamizi wa Sekta ya Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizaya ya Fedha Bw. Santley Kibakaya na Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Bi. Angela Mollel.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Bw. Msongela Palela, akizungumza na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambao walifika ofisini kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani Mara.

Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Bi. Angela Mollel (kushoto) na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Suguti, Bw. Joel Samson, wakimkabidhi fulana mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Suguti, Alex Baraka, baada ya kujibu swali kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Suguti mkoani Mara.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha wakazi wa Kijiji cha Suguti wakifuatilia elimu iliyotolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanznaia (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Suguti, Musoma, mkoani Mara.
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bi. Elizabeth Mzava, akitoa elimu ya fedha kwa wakazi wa Kijiji cha Suguti, elimu ya fedha inatolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanznaia (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC, mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Suguti, Musoma, mkoani Mara.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Mara).
……..
Na. Josephine Majura WF, Mara
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, Bw. Msongela Palela, amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kutumia mikopo wanayokopa kufanya uwekezaji unaozalisha faida ili kuepuka kushindwa kufanya marejesho ya mkopo.
Bw. Palela alitoa rai hiyo wakati alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Taasisi za Serikali na Binafsi ambayo ipo mkoani Mara kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali.
“Kwenye Wilaya yetu kumekuwa na changamoto kwa wananchi wetu kuchukua mikopo na hawaendi kuwekeza kwenye maeneo ambayo yatazalisha faida ili watumie faida ile kufanya marejesho”, alisema Bw. Palela.
Aliongeza kuwa wananchi kukopa sio jambo baya lakini alitarajia mikopo hiyo iwasaidie lakini imekua tofauti kwa sababu haiendi kutumiwa katika shughuli za uzalishaji hivyo wanashindwa kufanya marejesho.
Bw. Palale alifafanua kuwa elimu ya fedha ni muhimu hivyo ni vyema Wizara ya Fedha ikahakikisha inawafikia wananchi wote na elimu hiyo iwe endelevu kwakuwa ina mchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi endapo itaeleweka kwa wananchi wote.
Aidha, alizitaka Taasisi za Fedha zinazojihusisha na utoaji mikopo, kufuata utaratibu na Sheria zilizowekwa na Serikali ili mikopo wanayotoa kwa wananchi iwasaidie na isiwe chanzo cha kuongeza tatizo kwa kuweka riba kubwa zisizolipika kwa urahisi.
“Naendelea kuwaomba watoa huduma za fedha kuwa waaminifu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania za kuwalinda watoa huduma na wateja.
Vilevile, aliwataka Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kujenga utaratibu wa kutumia Taasisi rasmi zinazotambuliwa na Serikali wanapohitaji mikopo, ili kuepuka udhalilishaji unaofanywa na Taasisi ambazo haziko rasmi na hazifuati utaratibu.
Bw. Palela aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuendelea kuwachukulia hatua watoa huduma wanaofanya biashara kinyume na utaratibu unavyoelekeza.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Bw. Mbagira Kajanja, aliishukuru Serikali kwa kuwapatia elimu ya fedha ambapo alieleza kupitia elimu hiyo imewafumbua macho na kuelewa baadhi ya taratibu ikiwemo kuwa na haki ya kusoma mkataba kabla ya kuchukua mkopo na kuelewa masharti ya mkopo na kujua viwango vya riba.
“Naamini baada ya elimu hii, tutabadilika na kutumia Taasisi rasmi zinazotambulika na Serikal, tutasoma mkataba kwa makini na kama hatujaelewa tutaomba tuelimishwe kabla ya kusaini”, alisema Bw. Kajanja.
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Sekta ya Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizaya ya Fedha Bw. Santley Kibakaya, alisema kuwa Wizara inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya fedha kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2930.
Alisema kuwa hadi sasa Wizara ya Fedha imetoa elimu ya fedha katika mikoa 15, ikiwemo mkoa wa Kagera, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Pwani, Morogoro, Rukwa, Lindi, Mtwara, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Mara.
Lengo la Wizara ni kwamba hadi kufikia mwaka 2025/2026 mikoa yote 26 ya Tanzania iwe imepata elimu ya fedha.