Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo, na Diaspora, Mhe. Neale Richmond, amehitimisha ziara yake nchini kwa kutembelea Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).
Ziara hiyo imelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ireland katika nyanja za teknolojia na nishati endelevu.
Akiwa DIT, Mhe. Richmond alitembelea Maabara ya Ubunifu wa Ufanisi wa Nishati, inayofadhiliwa na Serikali ya Ireland kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) inayolenga kusaidia uvumbuzi wa teknolojia ya Nishati safi ili kuchochea maendeleo endelevu na kuimarisha sekta ya nishati nchini.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Richmond alisifu ushirikiano uliopo na kusisitiza umuhimu wa teknolojia bunifu katika kukuza uchumi na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Pia aliwatambua wanadiaspora kwa mchango wao katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia ujuzi wao wa kimataifa.
Waziri huyo alithibitisha kuwa Ireland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za nishati, elimu na teknolojia kwa maendeleo ya pande zote mbili.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alibainisha kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Ireland katika miradi ya teknolojia na nishati endelevu unatoa fursa kwa wanafunzi na watafiti wa Tanzania kupata ujuzi wa kisasa na kushiriki katika ubunifu wa suluhisho za kitaifa na kimataifa.
Alisisitiza kuwa ushirikiano huu utaongeza tija katika sekta ya elimu na TEHAMA.
Mawaziri hao wamekubaliana kuendelea na mashauriano na kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza mifumo ya nishati endelevu, ambayo itachochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kiteknolojia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Waziri Richmond aliambatana na viongozi mbalimbali, akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, ambaye pia anawakilisha Ireland, Mhe. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan, na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme.
Mhe. Richmond alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku Tatu ambapo Alikutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alitembelea miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Ireland na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Dkt. Batilda Buriani na kutembelea Kitengo cha Saratani cha watoto cha Hospitali ya Taifa Muhimbili.