Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb), ametoa pole kwa kaya takribani 319 ambazo zimeathiriwa na upepo mkali ulioezua paa za nyumba zao katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.
Mheshimiwa Majaliwa alitoa pole hiyo kupitia simu aliyompigia Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, wakati akiwa katika ziara ya kutembelea na kujionea athari zilizowakumba wakazi wa kata za Shaban, Makongoro, na Amri Abedi, kufuatia mvua iliyoambatana na upepo mkali usiku wa Machi 24.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati timu ya tathmini ikiendelea na kazi yake ili kuhakikisha waathirika wanapata msaada stahiki. Vilevile, aliwasihi kushirikiana na vyombo husika vinavyosimamia zoezi hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi, aliwataka wakazi wa maeneo yaliyoathirika kuendelea kuwa na subira huku akiwapongeza kwa mshikamano waliouonesha, ikiwa ni pamoja na kusaidiana kuhifadhi ndugu zao waliopoteza makazi.
Pia, Kanali Mtambi alibainisha kuwa hakuna kifo kilichoripotiwa kutokana na tukio hilo, ingawa watu wanane wamejeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu.
“Tunamshukuru Mungu kwamba hadi sasa hakuna aliyepoteza maisha. Tunao majeruhi wanane ambao wanaendelea vizuri na matibabu. Nawashukuru sana wananchi kwa mshikamano wenu katika hili, endeleeni kudumisha umoja,” alisema Mkuu wa Mkoa.