Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeandaa futari kwa heshima ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa watoto yatima wa Kituo cha Mazizini na wazee wa Kituo cha Sebuleni. Hafla hiyo imefanyika leo, Machi 26, 2025, katika Kituo cha Wazee Sebuleni, Zanzibar.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, amelishukuru TTCL kwa moyo wake wa kujali jamii kwa kuandaa futari na kutoa zawadi kwa watoto yatima na wazee. “Michango yenu leo inaonesha mshikamano wa TTCL na jamii pamoja na kujali mahitaji ya wasiojiweza,” amesema Sheikh Wadi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee, Bw. Hassan Ibrahim Suleiman, amepongeza juhudi za TTCL kwa kuendelea kusaidia makundi maalum. “Hii sio mara yenu ya kwanza kutuonyesha wema; mnakuwa mfano wa kuigwa na makampuni mengine,” amesema Bw. Suleiman.
Kwa upande wake, Meneja Mkaazi wa TTCL Zanzibar, Bw. Hilaly Mwinyi, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na jamii ili kuhakikisha kuwa michango yake inawafikia wale wenye uhitaji zaidi. “Tunajitahidi sio tu katika kuimarisha mawasiliano na huduma za kidijitali nchini, bali pia katika kujenga jamii yenye mshikamano, huruma, na maendeleo endelevu,” amesema Bw. Mwinyi.
Ameongeza kuwa TTCL itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa jamii kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kusaidia watoto yatima, wazee, na makundi mengine maalum, kwa lengo la kuimarisha mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania.
Mbali na michango yake ya kijamii, TTCL imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha huduma za mawasiliano nchini. Kupitia uwekezaji wake katika miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, shirika hili limewezesha upanuzi wa huduma za intaneti kwa kasi ya juu, kufanikisha mawasiliano katika afisi za serikali, taasisi binafsi, na vijijini, hivyo kuchochea maendeleo ya kidijitali Tanzania.