Masatu Wanjara (kushoto) na mkewe, Sherida Musibha, kulia muda mfupi baada ya kupokea msaada wa vifaa saidizi kutoka The Desk &Chair Foundation, ili kuwawezesha kutembewa.Picha na Baltazar Mashaka.
……………
NA BALTAZAR MASHAKA, BUNDA
Wakazi wa Kijiji cha Guta, wilayani Bunda, Masatu Wanjara na mkewe, Sherida Musibha, wamepokea vifaa saidizi vya kuwasaidia kutembea, baada ya kukumbwa na changamoto ya maradhi ya miguu kwa zaidi ya miaka miwili.
Msaada huo wenye thamani ya sh. 250,000 umetolewa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation na kukabidhiwa leo kwa wanandoa hao, hivyo vitawasaidia kutembea kwa urahisi tofauti na awali.
Masatu ameeleza furaha yake kwa kupokea msaada huo na kumshukuru mfadhili kwa kuguswa kutoa vifaa hivyo,baada ya kutumia mikongojo kwa muda mrefu kutokana na maradhi hayo.
Amesema msaada huo umetokea katika kipindi muafaka kwani yeye na mkewe walikuwa wamesumbuliwa na maradhi ya miguu kwa zaidi ya miaka miwili,ameeleza kuwa alikumbwa na jeraha lililosababishwa na maradhi kwenye mguu wake wa kushoto, huku mkewe akitumia kiti cha miguu minne kumsaidia kutembea.
Hata hivyo, Masatu ameeleza kuwa licha ya kupokea msaada huo, bado anasumbuliwa na maradhi ya tumbo ambayo yanapozidi, humfanya kupoteza fahamu ambapo ameomba msaada kutoka serikalini kwa sababu yeye na mkewe ni wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80, hivyo anahitaji matibabu ya kibingwa.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Dk. Sibtain Meghjee, amesema kuwa alipokea picha kupitia WhatsApp ikimuonesha Masatu na mkewe wakikabiliwa na changamoto ya kutembea.
Ameeleza kuwa taasisi yao inatoa msaada bila kubagua, kwa kuzingatia kauli mbiu yao ya “Iwe dhiki iwe faraja, tupo pamoja,” baada ya kuona picha hiyo, aliguswa na kutoa msaada wa vifaa saidizi vyenye thamani ya shi.250,000.
Dk. Meghjee amefafanua kuwa taasisi hiyo inajivunia kutoa misaada katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, maji, mikopo na ufugaji wa mbuzi, ili kusaidia watu wenye mahitaji na kupambana na umaskini.