Na mwandishi wetu
Benki ya NMB imeshiriki kikamilifu kama mdhamini wa Mkutano Mkuu Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), unaofanyika mjini Songea, mkoani Ruvuma. Mkutano huo muhimu kwa ukuaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kama mgeni rasmi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Balozi Dkt. Nchimbi aliwapongeza wahariri na kamati tendaji ya TEF kwa kuandaa uchaguzi wa viongozi kwa kuzingatia misingi ya haki na uhuru, akisema kuwa TEF ni mfano bora wa uongozi wa kikatiba nchini.
“Nawapongeza wahariri na kamati tendaji kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uchaguzi pamoja na kauli mbiu yenu ya Uchaguzi Huru na wa Haki. Kwa kufanya hivi, mnakuwa mfano wa pekee kwa nchi yetu,” alisema Balozi Dkt. Nchimbi.
NMB, ikiwa mdau muhimu wa maendeleo ya sekta ya habari nchini, iliwakilishwa katika mkutano huo na Meneja wa Kanda ya Kusini, Bi. Olipa Habeel. Uwepo wa benki hiyo katika mkutano huo unaonesha dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kujenga jamii yenye maarifa na uwazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alieleza mafanikio ya jukwaa hilo, likiwemo heshima ya kutoa Rais wa kwanza wa Wahariri Afrika Mashariki.
“TEF kwa sasa inatambulika ndani na nje ya nchi kutokana na kazi ya kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari. Heshima ya kuwa na Rais wa kwanza wa Wahariri Afrika Mashariki kutoka Tanzania ni ushahidi wa mchango wetu katika sekta hii,” alisema Balile.
Mkutano huo unatarajiwa kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wapya wa TEF na kujadili mikakati ya kuendeleza taaluma ya habari, licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wanahabari nchini.
Kwa ujumla, ushiriki wa NMB katika mkutano huu ni uthibitisho wa jinsi taasisi hiyo ya kifedha inavyoendelea kujenga mahusiano imara na wadau wa maendeleo, ikiwemo sekta ya habari, ambayo ni mhimili muhimu wa demokrasia na maendeleo ya taifa.