
NYARUGUSU, GEITA: Wanawake wa Kata ya Nyarugusu wamepumua kwa afueni baada ya Kituo chao cha Afya kupatiwa mashine ya kisasa ya ultrasound, hatua iliyowarahisishia huduma za afya ya uzazi ambazo hapo awali walilazimika kuzifuata mbali mjini Geita.
Hatua hiyo imekuja kama sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya nchini, kupitia uwekezaji wa vifaa tiba katika vituo vya pembezoni. Sasa, huduma za uchunguzi wa ujauzito kwa kutumia ultrasound zinapatikana moja kwa moja Nyarugusu — bila usumbufu wa kusafiri maili nyingi.
Katika kuadhimisha Wiki ya Wazazi, Jumuiya ya Wazazi ya CCM ilitembelea kituo hicho, ambapo walikagua huduma, kutoa zawadi kwa wagonjwa na kushuhudia mafanikio yaliyopatikana.
Barnabas Mapande, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, alisema:
“Haya ni matokeo ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, hata katika maeneo ya mbali.”
Paschal Mapung’o, Katibu wa Malezi na Mazingira wa Jumuiya hiyo, alieleza kufurahishwa na hali ya huduma kituoni, akisema sasa wanawake wanahudumiwa kwa heshima na ubora.
Albert Bayona, Afisa Tabibu wa kituo, alisema:
“Mashine hii ya ultrasound imekuwa msaada mkubwa, hasa kwa wajawazito. Tumepunguza vifo vya uzazi na kuchangia kwa kiasi kikubwa usalama wa mama na mtoto.”
Wanawake waliowahi kupata huduma kituoni hapo walielezea furaha yao, wakisema maendeleo hayo yameleta matumaini mapya katika maisha yao ya kila siku.