Na. Edmund Salaho – Mikumi
Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) leo Aprili 07, 2025 imeagiza kukamilishwa kwa miradi ya Miundombinu ya Utalii inayotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Mikumi haraka ili kuvutia watalii zaidi wanaotembelea Hifadhi hiyo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege Mikumi na miundombinu mingine ya malazi katika hifadhi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA
Jenerali (Mstaafu) George Waitara ameitaka Menejimeti ya Hifadhi ya Mikumi kuendeleza jitihada zinazofanyika za kuboresha miundombinu ya Utalii kwa kasi zaidi.
“Tumejionea uboreshaji wa miundombinu unaofanywa na Serikali hapa Mikumi ni dhahiri sasa Mikumi itaongoza katika Utalii wa ndani,” alisema Waitara
Aidha, Waitara aliitaka Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Mikumi kuhakikisha inawasimamia Wakandarasi ipasavyo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu ili kuendana na thamani ya pesa iliyotolewa na Serikali.
Naye, CPA Khadija Ramadhani Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini – TANAPA na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi na Utawala Bora aliishukuru Serikali kwa kutekeleza Miradi hiyo mikubwa ya kimkakati na kuitaka Menejimenti ya Mikumi kujipanga zaidi kuwahudumia watalii watakaofika katika maeneo ya Hifadhi.
“Mhe. Rais Samia amekwisha fanya kazi kubwa ya kutangaza maeneo haya ya vivutio pamoja na kuboresha miundombinu katika maeneo ya hifadhi, nisisitize Menejimenti ijipange vizuri katika kuwahudumia watalii katika maeneo yetu ya vivutio”
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa alibainisha kuwa mradi mkubwa unaotekelezwa na Serikali wa Reli ya SGR umekuwa chachu ya kuongezeka kwa watalii na mapato katika Hifadhi ya Taifa Mikumi na kwamba Shirika linajipanga kufungua lango jipya la Chamgore ili kutumia fursa ya uwepo wa treni hiyo kupitia kituo cha Kilosa.
“Hifadhi ya Taifa ya Mikumi inashuhudia mafanikio makubwa yanayotokana na utekelezaji wa Miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendeleza utalii hususani katika Hifadhi ya Taifa Mikumi imeleta matokeo makubwa katika mapato na kuongezeka idadi ya watalii “ alisema Kamishna Mwishawa.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye pia ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Augustine Massesa alibainisha kuwa miundombinu ya kisasa katika Hifadhi hiyo inaenda kuleta mapinduzi makubwa katika utalii hususani katika Kanda ya Mashariki.
“Ujenzi wa miundombinu ya kisasa unaofanywa na Serikali katika hifadhi hii ya Mikumi umeleta mapinduzi makubwa katika utali wetu. Mabadiliko haya ni ya kihistoria. Hapo awali tulikuwa tukipokea ndege ndogo 7 kwa siku, lakini sasa tunapokea ndege kubwa mpaka 15 kwa siku zenye uwezo wakubeba watalii 35 hadi 45”.
“Uwanja wa ndege wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, ambao unakaribia kukamilika, umechochea ongezeko la idadi ya wageni na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka hifadhi.
Kwa sasa hifadhi inapokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi, na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.” alisema Kamishna Massesa.
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha miundombinu katika maeneo yote ya Hifadhi za Taifa ambapo kupitia mradi wa REGROW, Hifadhi ya Taifa Mikumi zinajengwa Nyumba za kulala wageni (Cottages) tano, eneo la kutolea taarifa kwa watalli (VIC) katika lango la Kikoboga, Malango mawili katika eneo la Doma na Kikwaraza, Eneo ya kupumzikia wageni moja lililopo Mbuyuni, Kambi ya kulaza wageni pamoja na kuboresha uwanja wa ndege Kikoboga (Kikoboga Airstrip).