Mtafuti na Daktari bingwa wa watoto, Profesa Karimu Manji amehadharisha wazazi kutowaachia watoto wenye umri chini ya miaka mitano simu janja au vishikwambi kwa ajili ya kuangalia katuni kwamba inachangia kuwa na usonji.
Amesema dalili za usonji ni mtoto kuchelewa kuzungumza, kutokuangalia mtu usoni, hapendi kucheza na wenzake, kupata hasira kali au kuhisi msisimko anapokanyaga ardhini hivyo kutembelea vidole.
Pia mtoto huyo anakuwa na tabia ya kurudia vitu, kutamka maneno yasiyoeleweka tofauti na watoto wengine.
Akizungumza wakati wa kongamano la 15 la kisayansi lililofanyika jana katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Manji alisema wazazi wengi hudhani kwamba kumuachia mtoto simu ndio mapenzi badala yake wanaharibu watoto wao.
“Screen time kwa watoto chini ya miaka mitano ni hatari sana, mzazi jaribu kufuatilia hiyo katuni kwa kumuelekeza mtoto kila kinachofanywa na namna kinavyotamkwa. Kuwe na ufundishaji na sio kumtelekezea mtoto aangalie mwenyewe ili kumnyamazisha si sahihi,” alisisitiza.
Profesa Manji alisema vyakula vya kopo, dawa za kuua wadudu na za kufanya nyumba inukie, zinapaswa kutumiwa kwa uangalifu kwani zina athari kwenye ubongo wa mtoto.
Alisisitiza usonji hausababishwi na kurogwa, zongo au kurithi na kwamba tatizo hilo linahusu neva za fahamu ambalo mtoto anakuwa nalo hadi anapokuwa makubwa.
“Tusiwanyanyapae watoto hawa na tiba yao ni kuwagundua mapema na kuanza kuwapatia tiba ya matamshi na viungo ambazo gharama yake ni kubwa kwa siku ni 100,000 na kwa vile ni endelevu, wazazi wanafilisika tunahitaji mkakati wa makusudi katika sera zetu,” alisema.
Alisema kuwepo na walimu katika shule watakaosaidia watoto hao pamoja na tiba zipatikane kwenye bima kwani ni gharama kubwa.
“Wazazi msiwe wanyonge, watoto hawajarogwa. Wanaweza kubadilika tabia na kuwa wataalamu bingwa au wenye kuaminika katika jamii,” alisema.
Aliongeza mtu mwenye usonji awapo kazini hulalamikiwa kwa kutochangamana na watu, kuwa mtaratibu kupitiliza na kufanya mambo yake binafsi.