Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) CPA. Habibu Suluo akizungumza jambo leo Aprili 14, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari.
Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri akizungumza leo Aprili 14, 2025 jijini Dar es Salaam na wahariri wa vyombo vya habari.
Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bakari Kimwaga akizungumza jambo leo Aprili 14, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari.
Mwakilishi wa Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Revocatus Kasimba akizungumza jambo leo Aprili 14, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkuano na wahariri wa vyombo vya habari.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kutoa leseni 108,658 za usafirishaji pamoja na kuboresha usafiri wa umma nchini.
Akizungumza leo Aprili 14, 2025 jijini Dar es Salaam na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) CPA. Habibu Suluo, amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Februari 2021 hadi machi 2025 wamefanikiwa kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kutoa leseni za usafirishaji.
CPA. Suluo amesema kuwa leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo, huku vyombo vya usafiri wa kukodi ziliongezeka kutoka 226, 201 kwa mwaka 2020/21 hadi 334,859 kwa mwaka 2024/25.
“Ikiwa ni ongezeko la leseni 108,658 sawa na ongezeko la asilimia 48 ambapo ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne” amesema CPA. Suluo.
CPA. Suluo amesema kuwa pia wamefanikiwa kuanzisha njia mpya 1,007 za daladala Mkoa wa Dar es Salaam ili kufikia maeneo yasiyofikika pamoja na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kupunguza gharama kwa wananchi.
Amesema kuwa miongoni mwa njia zilizorefushwa kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam ni Mbezi Luis – Kisarawe kupitia barabara ya Malamba mawili na Banana.
Njia nyengine ni Toangoma – Pugu kupitia barabara ya Kilwa, Kivukoni – Bunju kupitia barabara ya Bagamoyo, Gerezani – Bunju Sokoni kupitia barabara ya Bagamoyo, Buyuni – Stendi kuu ya Magufuli kupitia kinyerezi.
Bunju Sokoni – Stendi kuu ya Magufuli kupitia Madale, Mbande Kisewe – Gerezani kupitia barabara ya Kilungule, Chang’ombe, Usalama, Mvuti – Machinga Complex pamoja na Tabata Segerea.
Ngobedi B- Machinga Complex kupitia Nyota Njema, pamoja Kitonga Gerezani kupitia barabara ya kilwa.
CPA. Suluo amesema kuwa katika Mkoa wa Arusha wamefanya mabadiliko ya njia ya daladala kwa kuzifanya baadhi ya njia kuwa na mzunguko kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo.
Amesema kuwa jiji la Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi, wameanzisha njia ya mpya kwa ajili ya kuyafikia maeneo mapya kutokana na kukua kwa kasi katika jiji hilo.
“Mfano wa njia hizo Machinga Complex – Mpamaa, Machinga Complex – Chidachi, Machinga Complex – Mpamaa Complex – Nzuguni, Machinga Complex – swaswa na vyakula vyao.
CPA. Suluo amefafanua kuwa hatua ya kuhamisha daladala kituo cha Machinga Complex imesaidia kuwepo kwa njia za mzunguko katikati ya jiji la Dodoma na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Mwakilishi wa Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Revocatus Kasimba, amesema kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari ili kuhakikisha malengo kusudiwa yanafikiwa kwa wakati.
“Vyomba vya habari mna jukumu kubwa la kuhamasisha uchaguzi, amani pamoja na usalama kwa watanzania wote” amesema Kasimba