Na Baltazar Mashaka, Mwanza
KATIKA juhudi za kulea kizazi chenye maadili na hofu ya Mungu, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,leo limewazawadia vijana walioshiriki mashindano ya kuhifadhi Qur’an zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitungi ya gesi na fedha taslimu.
Washindi sita wa mashindano hayo walipewa zawadi hizo,huku washiriki wengine 12 wakituzwa pia kama njia ya kuwahamasisha na kutambua juhudi zao za kuipenda na kuihifadhi Qur’an tukufu.
Lengo kuu la mashindano hayo ni kuwajengea vijana uwezo wa kuielewa Qur’an,kuipenda na kuihifadhi, sambamba na kuwalea katika maadili mema na maisha ya uadilifu.Watoto wanaofundishwa Qur’an wanajengwa kuwa raia wema, waaminifu na wenye hofu ya Mungu hata wanapopata ajira au madaraka.
Zawadi Zenye Maana Zaidi ya Mashindano
Kwa mujibu wa Sheikh Kabeke, zawadi ya mitungi ya gesi ni ya kihistoria na mkakati wa kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, na badala yake kutumia nishati safi kama gesi, ili kulinda mazingira na kupunguza uchafuzi wa hewa ukaa.
“Tunahamasisha utunzaji wa mazingira kama sehemu ya mafundisho ya Qur’an. Kupika kwa kuni na mkaa kunaharibu mazingira. Hii ni njia ya kushiriki kwa vitendo katika kulinda dunia yetu,” alisema Sheikh Kabeke.
Aidha, ameeleza kuwa mitungi hiyo ya gesi imetolewa kupitia msaada wa Zakaria Nzuki, ambaye amekuwa akimuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi an hewa ukaa (chafu),hadi sasa zaidi ya mitungi 70 imetolewa kwa jamii mbalimbali.
Ziara ya Kisiwa cha Saanane: Elimu Nje ya Darasa
Sheikh Kabeke alisema katika kuongeza hamasa na uelewa wa watoto kuhusu utalii wa ndani, aliwaahidi washindi hao safari ya kutembelea Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane ili kujifunza kuhusu wanyama na vivutio vya asili vya Tanzania.
“Tunahitaji kuwajenga watoto wetu wapende nchi yao na kutambua uzuri wa mazingira na rasilimali tulizopewa na Mungu. Hii itawasaidia kuwa raia wanaojali mazingira yao,” amesema na kuongeza kuwa,ziara hiyo pia inaunga mkono jitihada za Rais Samia kupitia filamu ya The Royal Tour, ambayo ililenga kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kwa dunia nzima.
Dini na Mazingira: Mafundisho ya Kidini Kwa Vitendo
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally Mbwana amekuwa akihimiza utunzaji wa mazingira kwa kuhimiza upandaji miti nchini kote., hivyo BAKWATA Mwanza imefanya kwa vitendo kwa kuweka mkakati wa kupanda miti kila wilaya ili kulinda mazingira na kutekeleza mafunzo ya dini kwa vitendo.
Katibu wa Umoja wa Walimu wa Madrasa (UWAMA) Mkoa wa Mwanza, Amani Ibrahim amesifu juhudi za BAKWATA na wadau, akieleza kuwa utoaji wa zawadi hizo ni kutimiza ahadi kwa washindi na ni fursa ya kuonesha fadhila kwa jamii ya Kiislamu.
“Mikakati yetu tunawafundisha watoto si tu kuhifadhi Qur’an bali pia kuwalea na kuwajenga katika maadili mema wae an hofu ya Mungu. Tunaamini Qur’an inawajenga watoto kuwa na misingi imara ya maisha.”
Ushirikiano wa Wadau
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha BAKWATA Online, Musabila Raphael, amesisitiza kuwa zawadi hizo ni kichocheo kwa watoto kupenda Qur’an na kuielekeza katika maisha yao.
“Kumlea mtoto na kumpa mapenzi ya Qur’an kutamfanya awe raia mwema,ni njia bora ya kupandikiza maadili ya uadilifu na hofu ya Mungu mapema,” amesema Raphael.
Pia amepongeza Umoja wa Walimu wa Madrasa kwa kuandaa mashindano hayo na kuhimiza mikoa mingine kuiga mfano huo ili kujenga taifa lenye misingi ya imani, maadili na uzalendo wa kweli.
Tukio hilo ni kielelezo cha jinsi dini, elimu na mazingira vinavyoweza kushirikiana katika kuijenga jamii bora, hivyo endelea kutembelea blogu hii kwa habari zaidi zenye kugusa jamii na kuinua maadili ya kizazi kijacho.1.Pic.86-Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani kabeke,leo akizungumza na waandishi wa habari, leo baada ya kutimiza ahadi ya kuwatunuku vijana walioshiriki mashindano ya kuhifdhi Qur’an.
Iqram Idd, akipokea zawadi ya mtungi wa gesi na bahasha ya fedha baada ya kuibuka mshindi wa kuhifadhi Juzuu Nne za Qur’an.
Mgeni rasmi Musabila Raphael , akizungumza kabla ya kuwakabidhi washindi wa Qur’an, zawadi leo.
Katibu Mkuu wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Chanila, akitoa ufafanuzi kuhusu zawadi kwa washindi na washiriki wa mashindano ya kuhifadhi Qur’an.