Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 19 Aprili 2025, amezindua gari la kubebea wagonjwa (ambulance) lililotolewa na Serikali kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mwakibete, jijini Mbeya. Uzinduzi huo unalenga kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wakati kwa wakazi wa Jiji hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Tulia amewashukuru Viongozi wa Serikali kwa kuendelea kupeleka huduma muhimu kwa wananchi, huku akiwataka wakazi wa Jiji la Mbeya kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na kumpigia kura kwa kishindo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ishara ya kutambua na kuunga mkono kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika kuboresha maisha ya Watanzania.