Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza,Sheikh Hasani Kabeke, akizungumza katika Kongamano la kuelimisha tunu za Taifa kwa viongozi wa dini na wadau,mkoani humu, leo Pigeon hotel.
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza,,Askofu Dk. Charles Sekelwa akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wadau, leo wakati wa kongamano la kuelimisha tunu za taifa kwa viongozi hao, lililofanyika Pigeon hoteli mkoani humu.
Mgeni Rasmi wa Kongamano la kuelimisha tunu za Taifa kwa viongozi wa dini na wadau,mkoani humu, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Changu Ng’oma (katikati walioketi mbele), katika picha ya pamoja na kamati ya amani ya Mkoa wa Mwanza.
Viongozi wa Dini Wilaya ya Nyamagana wakiwa katika picha ya mapoja leo, na mgeni rasmi katika kongamano la kuelimisha tunu za taifa, lililofanyika Pigeon hotel. (Picha na Baltazar Mashaka)
…….
2025
Na BALTAZAR MASHAKA,MWANZA,
Viongozi wa dini mkoani Mwanza wamewataka Watanzania wote, hususan wanasiasa na vyombo vya dola, kuheshimu na kuenzi tunu za taifa ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Wito huo umetolewa katika kongamano la amani lililowakutanisha viongozi wa dini, wanasiasa, vyombo vya ulinzi na usalama, waendesha bodaboda na machinga.
Tunu saba zilizosisitizwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na matumizi ya lugha ya taifa. Kwa mujibu wa viongozi hao, utekelezaji wa tunu hizo kwa vitendo ni msingi wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, usawa na bila migogoro ya kisiasa.
Sheikh Hasani Kabeke, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, ameeleza kuwa matumizi ya lugha chafu, matusi, na upendeleo kutoka kwa vyombo vya dola ni mambo yanayoweza kuchochea machafuko huku akionya kuwa siasa siyo mchezo wa kudhalilisha bali ni njia ya kuwahudumia watu kwa heshima na utu.
“Mwanasiasa anapotoa lugha za kudhalilisha, hata kwa wafu, anakiuka tunu ya utu. Rushwa na matumizi mabaya ya vyombo vya dola ni hatari kwa uadilifu wa uchaguzi,” ameonya Sheikh Kabeke, akitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi kuhakikisha uwazi na kutotumiwa kuvuruga uchaguzi.
Aidha, alikemea matumizi ya vijana kwa ajili ya kuchochea vurugu, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa kudai haki katika jamii.
Kwa upande wake, Askofu Dk. Charles Sekelwa, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, ameisitiza kuwa ukosefu wa uwazi, ushirikishwaji na uadilifu ni kiini cha migogoro mingi ya kijamii na kisiasa.
Amewataka viongozi wa taasisi, serikali na dini kuonyesha mfano wa utiifu kwa Katiba na maandiko ya kidini kama njia ya kulinda tunu za taifa ili kuufanya uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu nchi ibaki salama.
“Kiongozi asiye mzalendo ni tishio kwa taifa. Mzalendo wa kweli yupo tayari kulinda nchi yake, dini yake, taasisi yake na jamii yake kwa gharama yoyote,” amesema Askofu Sekelwa, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi wa serikali kufuata sheria na katiba ya nchi.
Katika kongamano hilo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Changu Ng’oma, amehimiza wapiga kura kutokubali kushawishiwa na propaganda au ahadi zisizotekelezeka na kutoa rai kwa wananchi wasiuze utu wao kwa ahadi hewa na fedha kidogo,wawaulize wagombea maswali magumu kabla ya kuwapa dhamana ya uongozi.
“Elimu kuhusu tunu za taifa ni muhimu ishuke hadi ngazi ya familia. Tusiuze utu wetu kwa fedha au ahadi hewa,” amesema Ng’oma.
Naye Mchunguzi Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Nyamagana, Protace Andrew, amewataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwaelimisha wauamini wao madhara ya vitendo hivyo, akisisitiza kuwa rushwa ni tishio kubwa kwa uongozi bora na maendeleo ya taifa.
Washiriki wengine wa kongamano wamehimiza uanzishwaji wa elimu ya tunu za taifa kuanzia ngazi ya familia, mashuleni na katika jamii kwa ujumla. Pia waliitaka Takukuru kuhakikisha inashughulikia vitendo vya rushwa kwa usawa bila upendeleo wa vyama.