Baadhi ya Vijana wa kijiji cha Linda Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakijaza udongo kwenye Barabara ya Linda-Ndembo ambayo imeharibika vibaya kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha kwa wingi ili kuruhusu shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao kufanyika kwa urahisi.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga
BAADHI ya wananchi wa vijiji vya Linda na Liyombo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA)kuchukua hatua za haraka kutengeneza Barabara ya Litowo-Linda-Ndembo ili waweze kuondokana na kero kubwa wanazozipata ikiwemo kushindwa kusafirisha mazao kwenda sokoni.
Wamesema, kwa sasa barabara hiyo haipitiki kirahisi kutokana na kuharibika vibaya na mvua za masika zinazoendelea kunyesha kwa wingi ambazo zimesababisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa kutumia magari kusimama.
Joseph Mbele Mkazi wa kijiji cha Liyombo alisema,Wananchi wa kijiji hicho ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara ikiwemo,kahawa, mahindi,maharage na ndizi lakini wanashindwa kuyafikisha sokoni kwa wateja kutokana na ubora wa barabara.
“Kuna wanunuzi wanakuja katika kijiji cha Liyombo kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kama Mtwara na Lindi kuja kununua ndizi,lakini kipindi hiki hawafiki kwa sababu ya ubovu wa barabara hii”alisema Mbele.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Danfod Komba alisema,ubovu wa barabara umesababisha maisha yao kuwa magumu kwani licha ya kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara lakini wanashindwa kupeleka mazao sokoni kutokana na ubovu wa barabara.
Alisema,kutokana na ubovu wa barabara hiyo wanalazimika kuuza mazao yao yakiwa shambani kwa tena bei rahisi isiyolingana na gharama za uzalishaji ili kuepuka mazao kuoza badala ya kupeleka sokoni ambako watapata bei nzuri.
“Tunaiomba Serikali ichukue hatua za haraka kufanya matengenezo ya barabara hii inayotoka makao makuu ya kata kijiji cha Linda hadi Liyombo,kwani tunashindwa hata kusafirishamazao yetu kwenda sokoni”alisema Komba.
Katika kijiji cha Linda vijana waliojitolea kufanya matengenezo kwa baadhi ya maeneo ya barabara hiyo walisema,tangu mvua za masika zilivyoanza kunyesha mwezi Desemba hadi April zimeharib kabisa miundombinu ya barabara hiyo na kusababisha baadhi ya shughuli za maendeleo kusimama.
Elias Komba alisema,wameamua kufanya matengenezo ya barabara ili waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuruhusu shughuli za usafiri hasa kwa watoto na mama wajawazito kufika kwa haraka kwenye maeneo ya kutolea huduma za kijamii.
Alisema,kutokana na ubovu wa barabara hiyo wamiliki wa magari wamesitisha kupeleka magari yao kwa kuhofia usalama na kwa sasa wananchi wanategemea usafiri wa pikipiki pekee ambao ni gharama kubwa.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga Mhandisi Oscar Mussa alisema,wanatambua changamoto iliyopo katika barabara hiyo na kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga Sh.milioni 400 ili kujenga daraja la Ndembo katika mto Ngaka na kujenga barabara yenye urefu wa kilometa 13.
“Kwa sasa tunasubiri kupata idhini ya Serikali ili tuweze kufanya matengenezo,tunawaomba wananchi wawe wavumilimivu Serikali inatambua changamoto zilizopo katika barabara hiyo na itazifanyia kazi haraka iwezekanavyo”alisema Mussa.