KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, serikali ya mapinduzi Zanzibar Dk Islam Seif Katibu amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umelindwa na kutunzwa na waasisi pamoja na viongozi waliopo madarakani.
Akizungumza katika kongamano la miaka 21 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika katika Chuo cha Uhasibu kampasi ya Arusha(IAA) leo Dk Khatib amesema amesema Muungano umejengwa kutokana na mahusiano ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na undugu.
Kadhalika Dkt. Khatib ameipongeza menejimenti ya Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA), kwa namna inavyosimamia maendeleo ya chuo ikiwamo kupanua wigo kwa kujenga Kampasi ya IAA Zanzibar, kama juhudi za kutunza na kudumisha Muungano wa Tanzania.
“Ninawaahidi kuwa nitahakikisha maombi ya kupata eneo la kujenga Kampasi hiyo yanakamilika kwa haraka” amesema
Ametoa wito kwa wanataaluma na vyuo vingine kuwa na maono kama IAA katika kuhakikisha muungano unaendelea kutunzwa, na kupitia maono yao waweze kutafsiri umuhimu wa muungano kiuchumi, kisiasa, kijamii na kimazingira na kiteknolojia kwa kadri dunia inavyobadilika.
Awali Mkuu wa Chuo cha IAA Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema chuo kimekuwa na mahusiano mazuri na Zanzibar ambapo zaidi ya wanafunzi 100 hujiunga na chuo hichi kwa mwaka.
Amesema dhamira ya IAA ni kufungua Kampasi visiwani Zanzibar ili kufundisha fani zitakazoendana na mabadiliko makubwa yaliyopo.
Wahadhiri Waandamizi walioshiriki katika kongamano hilo akiwamo Dkt. Grace Idinga-Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa IAA amesema chuo kinafundisha, kutafiti na kushauri masuala mbalimbali ya muungano.
Wachangiaji wengine wametaja muungano kuwa umeleta ushirikiano katika elimu, biashara, ajira, umeondoa ukabila na kusisitiza utunzwe.