KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imezindua rasmi kampeni ya Kili Challenge 2025 ikiwa ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini. Mpango huu, unaoendeshwa kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), unalenga kuchangisha fedha za ndani ili kusaidia jitihada mbalimbali za kupambana na UKIMWI nchini kote.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Jerry Silaa aliipongeza GGML na TACAIDS kwa kuendeleza ushirikiano wao wa muda mrefu katika kuandaa kampeni hii, ambayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 imekuwa nguzo muhimu ya ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya huduma za UKIMWI.
“Kampeni hii si ya kuchangisha fedha tu, bali ni ya kuunganisha nguvu zetu kupunguza unyanyapaa unaohusiana na VVU, kuboresha upatikanaji wa matibabu, na kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu.
“Sote tumeshuhudia mageuzi makubwa ya Serikali ya Awamu ya sita ambapo uwekezaji mkubwa wenye matokeo umefanyika katika kuimarisha huduma za kinga, tiba na matunzo za VVU na UKIMWI, uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeweka kipaumbele cha kutokomeza UKIMWI hapa nchini ifikapo mwaka 2030”, aliongeza mheshimiwa waziri.
Mheshimiwa Waziri Silaa alisema kuwa takwimu zinaonesha matumaini makubwa kwa kupungua kwa maambukizi mapya kutoka watu 72,000 kwa mwaka (2016–2017) hadi watu 60,000 kwa mwaka (2022–2023).
“Huu ni ushahidi kwamba jitihada zetu zina matokeo, lakini safari bado ni ndefu maana hadi kufikia Desemba 2024, Tanzania inakadiriwa kuwa na takribani watu milioni 1.7 wanaoishi na VVU, ambapo zaidi ya milioni 1.5 tayari wanapata dawa za kufubaza VVU”, aliongeza mheshimiwa waziri.
Kili Challenge 2025 inakaribisha watu kutoka sekta zote kushiriki katika tukio la kuchangisha fedha kwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kufanya matembezi ya baiskeli kuzunguuka mlima huo. Hafla ya kuwaaga washiriki itafanyika tarehe 18 Julai 2025, ikifuatiwa na hafla ya kuwakaribisha wakati wakishuka mlima tarehe 24 Julai 2025 , Mkoani Kilimanjaro.
Kwa zaidi ya miaka 20, Kili Challenge imechangia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kusaidia miradi ya UKIMWI, ikiwalenga hasa watu wanaoishi na VVU, yatima, na jamii zilizotengwa. Fedha zitakazopatikana mwaka huu zitaelekezwa katika huduma za kinga, matibabu kwa watu wanaoishi na VVU, na uwezeshaji wa kiuchumi kwa makundi yaliyo hatarini zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Duran Archery, Meneja Mwandamizi wa Masuala ya Uendelevu, Gilbert Mworia alisema, GGML kama mdhamini mkuu wa tukio hili, imekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya kampeni hii na kusisitiza dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kuiunga mkono kampeni hiyo na kuonesha umuhimu wa sekta binafsi katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Akizungumzia Kili Challenge ya mwaka 2024 alisema jumla ya wapandaji mlima 42 na waendesha baiskeli 18 walishiriki katika safari hiyo ya kihistoria ya kupanda kilele cha Mlima Kilimanjaro na kuzunguka Kingo zake na juhudi hizo za kishujaa zilisaidia kupatikana kwa zaidi ya dola za Marekani 850,000 kutoka kwa mashirika, taasisi na watu binafsi.
“Fedha hizi zimechangia sana katika kusaidia miradi ya jamii inayowawezesha watu wanaoishi na UKIMWI, kutoa elimu na chakula kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, na kutoa ruzuku kwa miradi mbalimbali ya kitaifa na kijamii inayotoa huduma muhimu kwa waathirika wa janga hili.
“Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa michango yetu inaendelea kugusa maisha ya watu wengi, tupande pamoja, tuendeshe pamoja kwa ajili ya dhamira hii, kwa ajili ya taifa letu na kwa ajili ya mabadiliko. Tuko Pamoja, Tunaleta Mabadiliko, Usikate Tamaa”, alisema Mworia.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Catherine Joachim, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kati ya serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kiraia ili kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95 ambayo ni; 95% ya watu wanaoishi na VVU kujua hali zao, 95% ya wanaojua hali zao kuwa kwenye matibabu, na 95% ya walioko kwenye matibabu kufanikisha kudhibiti kiwango cha virusi mwilini (viral suppression).
“Serikali ya awamu ya sita (6) chini ya uongozi mahiri wa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kuimarisha na kuboresha huduma za VVU na UKIMWI nchini, hii ni pamoja na huduma za kinga dhidi ya VVU na huduma za matibabu ya maradhi ya UKIMWI, na kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya Upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI, kuendelea kuimarika kwa huduma za VVU na UKIMWI hapa inchini kumesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka watu zaidi ya 39,000 kwa mwaka 2017 hadi watu 25,000 mwaka 2024.
“Serikali imeendelea kuhakikisha huduma za VVU na UKIMWI zinapatikana nchini kwa makundi yote. Sambamba na mafanikio mengi yaliyopatikana, bado kuna baadhi ya makundi katika jamii yetu yapo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU na pia kuna upatikanaji hafifu wa huduma”, alisema Dkt. Catherine.
Aidha aliyataja makundi haya kuwa ni pamoja na jamii wa wachimbaji wadogo, jamii ya wavuvi, jamii zinazoishi pembezoni wa njia kuu za usafirishaji, vijana hasa wasichana na wanawake wanaofanya biashara ya ngono akiongeza kuwa uhitaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika makundi haya ni wa kipekee.
Uzinduzi wa Kili Challenge 2025 ni hatua ya kihistoria katika juhudi za kupunguza utegemezi wa Tanzania kwa wafadhili wa nje katika mapambano dhidi ya UKIMWI, na kuimarisha uwezo wa nchi kufadhili na kutekeleza mipango ya afya kwa kutumia rasilimali za ndani.
Tukio hili pia limeangazia umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha zitakazokusanywa. Washiriki walikumbushwa kuwa mapato yote yatadhibitiwa kupitia Mfuko wa Kili Trust Fund, kuhakikisha yanatumika kwa ufanisi na kuwafikia walengwa halisi.
Kampeni ya Kili Challenge 2025 itaendeleza utamaduni wa kuwakutanisha watu binafsi na taasisi mbalimbali kutoka Tanzania nzima kushiriki kwa pamoja katika jitihada za kupambana na UKIMWI, kwa kuongeza uelewa na kuchangisha fedha ili kuboresha maisha ya watanzania.
Meneja Mwandamizi Masuala ya Uendelevu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Bw.Gilbert Mworia akizungumza jijini Dar es Salaam jana, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2025, ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi. Kampeni hiyo inafanyika chini ya udhamini mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, akipokea begi kutoka kwa Meneja Mwandamizi Masuala ya Uendelevu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Bw. Gilbert Mworia, jijini Dar es Salaam jana, kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2025, ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi. Kampeni hiyo inafanyika chini ya udhamini mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML). Kulia ni
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (wa tatu kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni (wa pili kushoto), Meneja Mwandamizi Masuala ya Uendelevu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited Bw.Gilbert Mworia (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Time ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS)), Dkt. Catherine Joachim, wakishangilia jijini Dar es Salaam jana, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2025, ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi. Kampeni hiyo inafanyika chini ya udhamini mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited(GGML).
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa,na Meneja Mwandamizi Masuala ya Uendelevu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Bw.Gilbert Mworia, wakiwa katika hafla uzinduzi rasmi wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2025, ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi. Kampeni hiyo iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam jana, inafanyika chini ya udhamini mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining limited (GGML).
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (katikati), wawakilishi kutoka Geita Gold Mining Ltd, TACAIDS na wadau wengine, wakishangilia, jijini Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya mheshimiwa waziri kuzindua rasmi kampeni ya GGM Kili Challenge 2025, yenye lengo la kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi. Kampeni hiyo inafanyika chini ya udhamini mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining limited (GGML).
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, akishikana mikono na Meneja Mwandamizi Masuala ya Uendelevu wa Kampuni ya Geita Gold Mining, Bw.Gilbert Mworia (kushoto), jijini Dar es Salaam jana, katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2025, ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi. Kampeni hiyo inafanyika chini ya udhamini mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining limited (GGML).