Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kulia), akiwa na Makamu mpya wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, walipokutana na kufanya mazungumzo kwenye Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kushoto), ukiwa katika mazungumzo na Timu ya Benki ya Dunia ikiongozwa na Makamu mpya wa Rais wa Benki hiyo anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, kwenye Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Washington D.C, Marekani)
………..
Na Benny Mwaipaja, Washington D.C, Marekani
BENKI ya Dunia imeimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi wa nchi na kuwa nchi ya kupigiwa mfano barani Afrika licha ya misukosuko mbalimbali ya kiuchumi inayoikabili dunia.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu mpya wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwenye Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Dkt Diop alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO 19 na mizozo ya kisiasa inayoendelea sehemu mbalimbali duniani, tathimini ya Benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.
Alisifu pia mikakati iliyowekwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya Sera za nje za Marekani na duniani kwa ujumla za kupunguza misaada na kuondoa ufadhili katika miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, kwa kutumia fedha zake za ndani.
Aidha, alipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi itakayochochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alimweleza Makamu mpya wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, aliyechukua nafasi ya Bi. Victoria Kwakwa, aliyemaliza muda wake, kwamba Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania.
Alisema kuwa, usimamizi mzuri wa uchumi unatokana na mwongozo na maono makubwa ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania, ambaye ameelekeza fedha nyingi katika sekta za uzalishaji na maendeleo ya jamii lakini pia ujenzi wa miundombinu inayochochea ukuaji wa uchumi.
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuendelea kusimamia uchumi kwa kuimarisha sera za uchumi na fedha pamoja na kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi katika kujenga uchumi wa nchi pamoja na kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya mwelekeo ya kisera yanazotokea duniani ambayo kwa namna moja ama nyingine yameziathiri nchi nyingi za Afrika.
Uwekezaji wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania umefikia dola za Marekani bilioni 10.9 ambapo miradi 38 ya maendeleo inatekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, maji, elimu, nishati, ujenzi wa miundombinu ya Barabara, ujenzi wa masoko na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.