Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amewasisitiza wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Rais , wabunge na madiwani Utakao fanyika oktoba mwaka huu, kwa kuchagua viongozi bora watakaobeba shida za wananchi, kutumia haki yao ya kikatiba kugombea nafasi hizo pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo ni adui wa haki.
Mhe. Kasilda ametoa wito huo wakati wa Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya kuzaliwa kwa Dayosisi ya Pare, yaliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, Usharika wa Mwembe, kata ya Mwembe, wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
“Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Sisi kama kanisa tunayo dhamana kubwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu kwa kuombea uchaguzi huo ili uwe wa amani na utulivu, pamoja na kuhakikisha kwamba sisi waumini tunashiriki kwa kugombea na kupiga kura, maana ni haki yetu ya kikatiba”. amesema Mhe. Kasilda.
Aidha, amebainisha kuwa kushiriki vitendo vya rushwa katika uchaguzi kunaweza kusababisha kuchaguliwa kwa viongozi wasio na hofu ya Mungu, ambao hawatakuwa msaada katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Pia amewataka waumini kusimama na kuliombea Taifa ili uchaguzi huu ukawe huru na haki , lakini kumuombea kiongozi wetu mkuu Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ili Mungu aendelee kumpa afya njema, hekima na busara ili aweze kulivusha Taifa katika kipindi chote cha uchaguzi tukiwa salama.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, Mhe. Askofu Charles Mjema, alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Same kwa kushiriki katika maadhimisho hayo, huku akiwaasa waumini na wakazi wa Same kuwa wakarimu kwa watu wote.
Katika mahubiri yake, Askofu Charles Mjema aliwasisitiza waumini kumtumaini Mungu pekee na kutojiweka tegemezi kwa binadamu, lakini pi akasisitiza waumia kutoacha kushiriki uchaguzi huo kwani ni muhimu sana kwa mistakabali wa taifa letu .